NEWS

Wednesday 15 April 2020

Rais Magufuli atoa pole vifo vya watu 18 ajalini Pwani


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki wa watu 18 waliopoteza maisha katika ajali ya barabarani iliyotokea leo Aprili 15, 2020 saa 12:55 asubuhi katika kijiji cha Kilimahewa Kaskazini wilayani Mkuranga, Pwani.
 Ajali hiyo imehusisha basi dogo la abiria (coaster) lililokuwa likitoka kijiji cha Magawa wilayani Mkuranga kwenda jijini Dar es Salaam ambalo limegongana na uso kwa uso na lori la mizigo (scania) lililokuwa likitoka Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kusini.

 Rais Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo kufikisha salamu zake za pole kwa familia za marehemu na kueleza kwamba anaungana nao katika kipindi hiki cha majonzi ya kuondokewa na wapendwa wao.
 “Nawaombea familia za marehemu wote, ndugu, jamaa na marafiki kuwa na moyo wa uvumilivu na ustahimilivu katik kipindi hiki kigumu cha majonzi, kuwapoteza Watanzania wenzetu kwa idadi kubwa namna hii inaumiza sana,” amesema Rais Magufuli na kuombea roho za marehemu hao zipumzishwe mhali pema peponi na majeruhi wote wapone haraka na kuungana na familia zao. 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages