KANDA
ya Ziwa imejaaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii vinavyopatikana katika maeneo
mbalimbali zikiwemo Hifadhi za Taifa za Serengeti, Rubondo, Saanane na
Burigi-Chato.
Hifadhi
ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Kanda ya Ziwa inapakana na mikoa ya Mara na
Simiyu. Inaaminika ndiyo eneo la kwanza duniani
linalotambulika kama urithi wa dunia na hifadhi ya mazingira hai (Biosphere
Reserve).
Ndiyo hifadhi pekee duniani yenye makundi makubwa ya wanyama wahamao na
idadi kubwa ya wanyama walao nyama, nyasi na majani.
Kwa mujibu wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania
(Tanapa), Serengeti ni miongoni mwa hifadhi za zamani
sana barani Afrika na kituo muhimu cha ndege wa asili na wahamao kutoka nchi za
Kaskazini mwa dunia.
Mwaka
2015 hifadhi hii ilitangazwa na mtandao maarufu wa
kimataifa unaojulikana kwa jina la ‘Safaris Bookings’ kwamba ndiyo inayoongoza kwa kuwa na
vivutio bora vya utalii barani Afrika.
Kamishina wa Uhifadhi Tanapa, Allan Kijazi anasema uteuzi huo ulifanyika baada ya hifadhi hii kushindanishwa na hifadhi
nyingine 50 barani Afrika zikiwemo za Afrika Kusini.
Wanyama
wanaoipendezesha zaidi hifadhi hii ya Serengeti ni nyumbu na pundamilia wenye historia ya kipekee. Ukifika hifadhini utawaona wakiwa katika
makundi makubwa na misafara mirefu wakitafuta malisho na kufurahia mazingira
hai.
Mwongoza watalii katika hifadhi hii, Julius Muhale
kutoka kampuni ijulikanayo kama Serengeti Services,
anasema watalii wengi hupendelea kupelekwa maeneo yenye makundi na misafara ya
nyumbu na pundamilia.
Mmoja wa watalii wa ndani aliyezuru hifadhi hii
ya Serengeti hivi karibuni, Pinner Kiwia anaelezea kuvutiwa kwake na wanyama
hao, miongoni mwa wengine.
“Nimeona wanyama wengi lakini walionivutia
zaidi ni nyumbu na pundamilia. Ninatamani kurudi tena
kufurahia vivutio vya utalii katika hifadhi hii,” anasema Kiwia.
Mkoani Mwanza kuna Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha
Saanane. Hii nayo ina utajiri wa vivutio lukuki vya utalii ambavyo ni pamoja na wanyama
kama swala pala, fisi maji, mamba, pimbi, tumbili na kobe. Pia ndege wazuri wa
aina nyingi na nyoka wakiwemo chatu.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Saanane |
Unapokuwa ndani ya hifadhi hii pia unapata
fursa ya kuona mandhari nzuri ya asili yenye miamba mikubwa, vichaka, miti na
nyasi fupi, fukwe na uwanda mwanana wa Ziwa Victoria.
Mkoani Geita kuna Hifadhi ya Taifa
ya Kisiwa cha Rubondo. Hifadhi hii ni makazi na mazingira muafaka ya kuzaliana
kwa samaki wakiwemo sato na sangara.
Pia hifadhi hii ni maskani makuu ya
ndege wala samaki kama zumbuli (kingfisher), chechele (flycatcher) na taisamaki
(fish eagle).
Mbali ya ndege hao, kisiwa hiki ni makazi
ya aina nyingine nyingi za ndege wa majini na mimea mbalimbali inayotoa harufa
nzuri.
Baadhi ya anyama wakazi wa hifadhi
hii ya Rubondo ni viboko, pongo, nzohe, fisi maji, mamba na pimbi wanaoshirikiana
makazi na wanyama waliohamishiwa katika hifadhi hii kama sokwe, tembo, twiga,
mbega weusi na weupe.
Sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo |
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili
na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla, mpango wa wizara hiyo ni kuongeza vivutio vya
utalii, hasa wanyama wakiwamo faru kwenye hifadhi hii.
Dkt Hamisi Kigwangalla, Waziri wa Maliasili na Utalii Tanzania |
Kivutio kingine kikubwa cha utalii
katika kanda hii ni Ziwa
Victoria lenye ukubwa wa kilomita za mraba 68,800, ambalo ni la kwanza kwa
ukubwa Afrika na la pili kwa ukubwa duniani baada ya Superior lililopo
Marekani.
Ziwa
hili linapakana na mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Simiyu na Geita katika Kanda
ya Ziwa. Kwa upande mwingine, limetambaa kuunganisha nchi za Tanzania, Kenya na
Uganda.
Linabeba
rasilimali za samaki na maji baridi na ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa karibu nchi zote zinazounda Jumuia ya
Afrika Mashariki (EAC), yaani Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan
Kusini.
Kanda
ya Ziwa pia kuna Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambao ni sehemu ya vivutio vya
utalii katika kanda hii. Uwanja huu una sifa ya kipekee ya kijiografia ya kuwa
katikati ya Ukanda wa Maziwa Makuu unaoundwa na nchi 11.
Nchi
hizo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasi
ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Afrika ya Kati, Rwanda, Angola, Sudan na Zambia.
Kwa
mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania - TAA (www.taa.go.tz), uwanja huu wa
Mwanza ni wa tatu kwa ukubwa wa mindombinu ya kuhudumia ndege za abiria na
mizigo na kibiashara hapa nchini baada ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Kilimanjaro (KIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Ziwa Victoria mkoani Mwanza |
Pia
kuna Makumbusho ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere katika wilaya ya
Butiama mkoani Mara alikozaliwa na kuzikwa, Makumbusho ya Utamaduni wa Kabila
la Wasukuma Bojora na Soko la Kimataifa lenye maduka ya kifahari la Rocky City
jijini Mwanza.
Vivutio vingine vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa ni daraja la juu la wenda kwa miguu la Furahisha na ghorofa la kwanza kujengwa katika Afrika Mashariki la Nyanza lililopo jijini Mwanza.
Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere |
Vivutio vingine vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa ni daraja la juu la wenda kwa miguu la Furahisha na ghorofa la kwanza kujengwa katika Afrika Mashariki la Nyanza lililopo jijini Mwanza.
Vingine
ni bandari, kituo cha reli, makazi ya watu milimani, jiwe lililopo kisiwani
Ukerewe mkoani Mwanza linalodaiwa kucheza kila linapoimbiwa wimbo, Mto Mara na
chemichemi ya maji ya moto katika kijiji cha Majimoto wilayani Serengeti, Mara.
Utajiri
wa vivutio hivi vya utalii utakuwa na maana kama vitatangazwa kikamilifu na
kutembelewa na watalii wengi wa ndani na kigeni ili pamoja na manufaa mengine,
kuchangia ukuaji wa uchumi wa wananchi na taifa kwa jumla.
Mshindi
wa Tuzo ya Utalii wa Ndani kwa mwaka 2012 iliyotolewa na Tanapa, Phinias
Bashaya anasema kuzuru maeneo yenye vivutio vya utalii kunamwezesha mtu kuona
vitu ambavyo havipatikani uraiani.
“Mfano, unapotembelea hifadhi za taifa nchini
unajionea ikolojia, maisha ya wanyamapori, kujua umuhimu na mchango wake katika
maendeleo ya taifa letu,” anaongeza Bashaya.
Mhitimu
wa Chuo cha Uhifadhi wa Wanyamapori Mweka kilichopo Moshi mkoani Kilimanjaro,
Heriel Masaki, anasema “Ukitembelea maeneo ya vivutio vya utalii unapata nafasi
ya kuuliza maswali na kujibiwa kuhusu utalii na uhifadhi.”
Akizungumzia utalii wa ndani, Masaki anasema pia hushawishi
wananchi kuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi kuepusha uharibifu wa
mazingira na migogoro ya kuvamia maeneo ya hifadhi.
Mkazi
wa jijini Mwanza, Rehema Mang’era, anasema kuzuru maeneo ya vivutio vya utalii,
hususan katika hifadhi za taifa nchini kunambadilisha mtu kisaikolojia, ndiyo
maana hata shule za msingi, sekondari na vyuo mbalimbali vinaratibu safari za
wanafunzi wao kutembelea hifadhi hizi.
“Kwa
hiyo ni vizuri wananchi wote wajenge utamaduni wa kutembelea hifazi za taifa
nchini ili kujifunza mambo mengi ya utafiti na kihistoria ya wanyamapori,
ndege, wadudu, mimea na mazingira hai. Lakini pia wanasayansi wanasema ukiona
maua mazuri na wanyama unaongeza miaka yako ya kuishi duniani,” anasema
Mang’era.
Mtaalamu
wa tiba za wanyamapori, Dk Titus Kamani anasema kuna umuhimu wa Watanzania
kujenga tabia ya kutembelea hifadhi za taifa mara kwa mara ili pamoja na faida
nyingine, kupata fursa ya kujua tabia za wanyamapori, miongoni mwa viumbe hai
wengine.
“Watu wengi hawajui tabia za wanyamapori kwa sababu
hawatembelei hifadhi. Wanyama kama sokwe mmoja wao akifa huweka matanga,”
anasema Dk Kamani.
Mhifadhi Mkuu wa Tanapa, Kijazi, anaona umuhimu wa shirika hilo na wadau wengine kuongeza kasi
ya kuvitangaza vivutio vya utalii nchini vikiwamo hivyo vilivyopo Kanda ya Ziwa
ili watu wengi ndani na nje ya nchi wahamasike kuvitembelea.
Bodi
ya Utalii Tanzania (TTB) ndiyo yenye dhamana ya kuratibu safari za wadau
mbalimbali wanaokwenda kutangaza vivutio vya
utalii katika maonesho na masoko ya kimataifa.
Msimamizi
wa TTB Kanda ya Ziwa, Gloria Munhambo anasema juhudi zinazofanywa na Serikali
ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk Magufuli za kuwekeza kwenye sekta ya usafiri
wa anga kwa kununua ndege za masafa marefu, ni kichocheo cha shughuli za
utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo Kanda ya Ziwa na nchini kwa jumla.
Munhambo
anatoa wito kwa vyombo vya habari nchini kuunga mkono juhudi za TTB, Wizara ya
Maliasili na Utalii na serikali kwa jumla katika kutangaza vivutio hivyo ndani
na nje ya nchi ili kushawishi watu wengi kutoka pembe zote duniani kuvitembelea.
Matarajio
yake ni kwamba utangazaji wa vivutio vya utalii nchini utaendelea kufanyika kwa
umakini unaozingatia kulinda maslahi ya taifa ili kuepusha hali yoyote
inayoweza kukwaza watalii wa ndani na kigeni wenye nia ya kuzuru maeneo
yanayovihifadhi.
(Imeandikwa na Christopher Gamaina)
Nimejifunza vingi
ReplyDelete