WAKATI bhaadi ya watu duniani wapo kwenye zuio la kutoka
ndani ya nyumba zao, takwimu zinaonesha mpaka sasa vifo vinavyotokana na virusi
vya corona ni mara 10 ya vile vilivyosababishwa na homa nyingine za mafua
ikiwemo SARS na MERS.
Wanasayansi
na watafiti wanahangaika kuhakikisha kwamba wanasaidia dunia kurudi kwenye hali
ya kawaida kwa kugundua chanjo itayotukinga dhidi ya corona, ukiacha njia
zisizohusisha dawa ama zile za muda mfupi kama vile kunawa mikono, kuvaa
barakoa na kukaa umbali wa mita moja kati ya mtu una mtu.
Chanjo
ya maabara ina hatua nyingi za kitafiti kabla ya kukubalika kwamba ni salama
kwa matumizi ya binadamu na mpaka sasa taarifa zinaonesha upatikanaji wake ni
kuanzia mwisho wa mwaka huu.
Kwa
kulitambua hili, kuna nchi kama Sweden zimeamua kutegemea kinga ya jumla ya
mwili ijulikanayo kitaalamu kama “herd immunity” kama njia mojawapo ya
kupambana na janga la corona mpaka pale chanjo itakapopatikana.
Wao
hawajaweka nchi yao kwenye zuio la raia wao kutoka ndani ya nyumba zao, lakini
wananchi wanatakiwa kufuata ushauri wa kitaalamu kuzuia maambukizi huku wale walio
kwenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya corona wakiwamo wazee na wenye
magonjwa suku wakihimizwa kukaa nyumbani.
Hata
kabla ya ujio wa virusi vya corona, aina hii ya kinga imetumika/kuhusishwa na
hatua za kumudu magonjwa mengine ya kuambukizwa ikiwemo polio, surua,
tetekuwanga, n.k.
Sasa
tuangalie ni kwa namna gani kinga hii ya jumla inafanya kazi katika jamii.
Kinga ya jumla
ya mwili ni nini?
Virusi
vya SARS-CoV-2 vinavyosababisha corona vilipoanza kusambaa hakuna mtu aliyekuwa
na kinga dhidi yake, hivyo havikupata upinzani wowote kuingia kwenye mwili wa
binadamu hali iliyovifanya kusambaa kwa haraka.
Watu
wengi wanapoendelea kuambukizwa, wengine hutengeneza kinga dhidi ya virusi hivi
na idadi ya walioambukizwa na waliotengeneza kinga wanapoongezeka basi jamii nzima
inapata kinga na hii ndio hujulikana kama kinga ya mwili ya jumla kitalaamu Herd Immunity.
Kinga
hii ya jumla ya mwili inapatikana pia pale ambapo watu wengi kwenye jamii
wamepata chanjo na hivyo kutengeneza kinga dhidi ya ugonjwa fulani ila kwa sasa
haiwezekani kwa kuwa chanjo ya virusi vya corona bado haijapatikana.
Taarifa
za awali za kisayansi zinatuonesha kwamba iwapo asilimia 70 ya watu watapata
maambukizi ya virusi vya corona na kutengeneza kinga basi asilimia thelathini
waliobaki watakingwa pia.
Swali
lako msomaji hapa litakuwa - hii inawezekana vipi?
Unaposema
asilimia 70 inamaana kwamba ukiwa na watu saba kati ya 10 wameambukizwa na wana
kinga inamaana usambazaji wa virusi utapungua maana hata kama watakuwa katika hatari
ya kupata virusi vya corona hawatapata maambukizi na wasipopata nao hawataweza
kuambukiza wale watatu waliobaki ambao hawana kinga, hivyo kusimamisha mzunguko
wa maambukizi.
Changamoto
ya aina hii ya kinga wakati chanzo za maambukizi ni kirusi ni kwamba virusi
vina tabia ya kubadilika vinasaba vinavokitengeneza na kuwa kipya kabisa.
Hivyo
basi, kinga zake zinakuwa za muda mfupi na kinga ya aina moja ya kirusi
haimaanishi ni kinga ya aina nyingine ya kirusi hata kama ni familia moja.
Mfano,
mtu aliyepata kinga dhidhi ya SARS-CoV inayosababisha SARS haimkingi mtu na
SARS-CoV-2 ingawa virusi vyote vinatoka kwenye familia ya corona.
Kupitia
tafiti inaonekana wazi kwamba kinga ya kawaida ya mwili dhidi ya homa, mafua
bila chanjo inadumu chini ya mwaka mmoja. Iwapo kinga dhidi ya virusi vya
corona ni kama hizi basi inatarajiwa kwamba kinga hii itadumu kwa miezi kadhaa
au miaka lakini sio kwa maisha yote, hivyo kuongeza umuhimu wa kupatikana kwa
chanjo.
Tutarajie nini
miezi ijayo?
Wanasayansi
wanafanya kazi usiku na mchana ili chanjo ipatikane na watu wapate kinga dhidi
ya virusi vya corona.
Wakati
tukisubiria upatikanaji wake, kila mmoja wetu afanye sehemu yake kuhakikisha
usalama wake binafsi, usalama wa familia yake na Tanzania yetu. Sote kwa jumla
tuchukue tahadhari kama tunavyoshauriwa na wataalamu wa afya.
Na Daktari Shally Zumba Mwashemele
Simu: +255 716 615 651 Barua Pepe: shallyzumba@gmail.com
No comments:
Post a Comment