NEWS

Monday 4 May 2020

Ushauri wa kitabibu kuhusu COVID-19


 UGONJWA wa corona ama unavojulikana kitaalamu “COVID 19” ni mpya unaosababishwa na kirusi kipya kutoka kwenye familia kubwa ya virusi vya corona.

Virusi hivi vinaweza kusababisha magonjwa kwa wanyama na binadamu. Kwa binadamu, virusi mbalimbali vya Corona vinajulikana kusababisha maambukizi kwa njia za hewa ikiwemo mafua ya kawaida, MERS na SARs.

Tafiti nyingi zinaendelea kote duniani na mengi bado yanaendelea kugundulika kuhusu kirusi hiki kipya, lakini mpaka sasa sayansi inatuambia kirusi hiki kinaambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye maambuki kwenda kwa mwingine kupitia matone madodo madogo kutoka puani au mdomoni pale mtu mwenye maambukizi ya corona anapopiga chafya, kukohoa au kuongea.

Matone haya ni mazito, hivyo hushindwa kusafiri mbali. Pia yanaweza kudondokea kwenye vitu na sehemu kama meza na kitasa.

Kupitia tafiti, imegundulika kwamba virusi vya corona winaweza kuishi mpaka saa 72 kwenye plastiki na chuma kisichoshika kutu, chini ya saa 24 kwenye mbao na chini ya saa nne kwenye bati.

Mtu anaweza kuambukizwa corona iwapo atakuwa karibu na mtu mwenye virusi hivyo au akishika sehemu ambazo matone yenye virusi yamedondokea.

Ugonjwa huathiri umri na rika zote, ingawa watu wenye umri mkubwa/wazee, wale wenye magonjwa sugu kama pumu, kisukari, presha ya juu, magonjwa ya figo, matatizo ya mapafu au wenye saratani wana hatari kubwa zaidi ya kupata ugonjwa wa COVID-19 na unaweza kusabaisha kifo.

Kila mtu kwenye jamii ana wajibu wa kuchukua hatua na kujilinda.

Dalili za ugonjwa wa Corona ni pamoja na homa kali, kikohozi kikavu na kuchoka. Wagonjwa wengine hupata mafua, maumivu yakichwa, mwili na kuharisha.

Inachukua kati ya siku mbili mpaka 14 kwa mtu aliyeambukizwa ugonjwa wa corona kuonesha dalili yeyote kati ya hizi zilizotajwa.

Mpaka asilimia 80 ya watu wanaopata corona wanakuwa na dalili ndogo au hawana dalili kabisa, asilimia 15 wana dalili za kati na asilimia tano wanakuwa na dalili kali ikiwepo shida kubwa ya kupumua mpaka kuhitaji huduma za wagonjwa mahututi (ICU) na msaada wa kupumua kupitia mashine ambazo kitaalamu zinaitwa ventilators.
Mashine zinazotoa msaada wa kupumua kwa wagonjwa (Ventilators) (Picha kwa msaada wa mtandao)
Ni muhimu kuzingatia kwamba, haijalishi ufinyu wa dalili, mtu yeyote mwenye maambukizi ya corona hata kama hana dalali ana uwezo wa kuambukiza wengine.

Pindi utakaposikia dalili hizi tafuta msaada wa haraka kwenye hospitali iliyopo karibu yako ama piga 199 kupata ushauri wa kitabibu zaidi.

Virusi vya corona mwilini hushambulia mfumo wa hewa, hasa vifuko vidogo vidogo vilivyoko kwenye mapafu viitwavyo alveoli ambavyo kazi yake kubwa ni kusafirisha damu na kuhakikisha inakuwa na oksijeni ya kutosha.

Hata bila kuumwa, unavyotoa hewa ndani, alveoli zinajaa oksjeni na inapeleka hiyo oksijeni kwenye damu na unapotoa hewa nje, alveoli zinajikunja na zinatoa hewa ya kaboni dayoksaidi.

Vifuko hivi vinaathirika pale mtu anapopata virusi vya corona, uwezo wa mapafu kuhakikisha oksijeni inaingia kwenye damu na kaboni dayoksaidi inatolewa nje unapungua.

Mgonjwa huanza kuhisi hewani finyu na mwili kufanya kazi ya ziada kuvuta hewa kwa nguvu zaidi, hii ndio shida kubwa inayowakumba wagonjwa wa corona na kwa wengine mpaka kusababisha kifo.

Lakini taarifa za kisayansi zinaonesha kwamba, kuna watu ambao wanapungukiwa oksijeni mwilini lakini hawaoneshi dalili zozote kitaalamu wanaitwa “Silent Hypoxia” na hili ndilo kundi la hatari maana wanakufa kimya bila kujitambua.

Mpaka sasa, corona haina dawa wala chanjo, kilichopo ni kinga tu.

Katika kujikinga, Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri kuhakikisha tunaweka umbali wa kiasi cha mita moja mpaka tatu kati ya mtu na mtu, ili mtu akiongea, akikohoa au akipiga chafya matone yenye virusi hayamkuti aliye karibu naye.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus (Picha kwa msaada wa mtandao)
 Pili, kuhakikisha unatumia barakoa unapokuwa nje ya nyumba yako kwani virusi vinakaa mpaka saa tatu kwenye hewa.

Tatu, osha mikono na maji yanayotirirka na sabuni mara kwa mara na jiepushe kugusagusa uso wako mara kwa mara kwa mikono.

Nne, kupunguza mizunguko isiyo na lazima, rudi nyumbani baada ya kazi, epuka maeneo ya misongomano.

Tano, tumia vyakula vya kuimarisha kinga ya mwili ikiwepo matunda na mboga za majani zenye vitamini C kwa wingi ikiwepo brokoli, hoho nyekundu, machungwa, malimau.

Ningependa kufafanua kitaalamu umuhimu wa kuosha mikono kwa maji yanayotirika. Hii ni njia madhubuti sana ya kujikinga na gonjwa la corona.
Kirusi cha corona kimetengenezwa na vinasaba ambavyo vimefungwa kwenye ukuta wa mafuta. Sabuni, inaharibu huu ukuta wa mafuta na kufanya kirusi kibomoke na kisiwe na madhara tena.
Picha ikionyesha namna ya kunawa mikono kwa maji yanayotiririka (Picha kwa msaada wa mtandao)
Unaponawa mikono na maji yanayotiririka vile virusi vilivyokufa vinatoka kabisa mikononi mwako, na hii ni sababu inayofanya kunawa mikono na maji yanayotirika kuwa njia bora zaidi ya kuhakikisha usafi na usalama wa mikono yako kuliko hata kutumia kipukusi (hand sanitizer).

Unapotumia kipukusi, ingawa virusi vinakufa lakini vinabaki mikononi mwako mpaka pale utakapoosha mikono yako.

Nitoe rai, tuenendelee kujikinga na kufuata masharti na maelekezo yote yanayotolewa na wataalamu wa afya na mamlaka za afya za serikali.

Na Daktari Shally Zumba Mwashemele
Simu: +255 716 615651 Barua Pepe: shallyzumba@gmail.com


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages