Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Henry Mwaibambe, akionesha waandishi wa habari (hawapo pichani) nyamapori iliyokutwa ikisafirishwa na watuhumiwa watatu. |
JESHI la Polisi mkoani Simiyu linawashikilia watu watatu waliokutwa na nyara za serikali kinyume cha sheria za nchi.
Wanaoshikiliwa ni Saguda Limbu (20) mkazi wa Mwasilimbi, Saguda Nila (18) na Juma Bayege (21) wakazi wa Ihusi waliokutwa wakiwa na nyama ya wanyamapori yenye uzito wa kilo 124.5 na pikipiki aina SAN LG waliyotumia kusafirishia nyara hizo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Henry Mwaibambe, amewambia wanahabari ofisini kwake leo Jumamosi Agosti 29, 2020 kwamba polisi wamewakamata watuhumiwa hao kwa kushirikiana na askari wa pori la akiba la Maswa jana katika kijiji cha Mwasilimbi wilayani Bariadi.
“Watuhumiwa hawa tunawashikilia kwa makosa ya kujihusisha na ujangili wa wanyamapori na kukutwa na nyara za serikali bila kibali katika makazi yao,” amesema Kamanda Mwaibambe.
Kamanda Mwaibambe (kulia) akionesha wanahabari (hawapo pichani) pikipiki iliyotumiwa na watuhumiwa kusafirisha nyara za serikali kinyume cha sheria za nchi.
Kamanda Mwaibambe amefafanua “Watuhumiwa hawa walikutwa na nyama ya pundamilia kilo 109 na nyama kavu ya nyumbu kilo 15.5 kinyume cha sheria na pikipiki waliyokuwa wanaitumia kusafirisha nyama hizo."
Kwa mujibu wa Kamanda Mwaibambe, watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani keshokutwa Jumatatu kujibu mashtaka yanayowakabili.
(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Simiyu)
No comments:
Post a Comment