NEWS

Monday 3 August 2020

TIP yaibua kesi 100 za ukatili Kwimba

Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria Wilaya ya Kwimba, Mishano Sagalani

USHIRIKIANO wa Kiimani Tanzania (TIP) kupitia Mradi wake wa Boresha, umefanikiwa kuibua kesi zaidi ya 100 za ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto katika wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza, kati ya Januari na Julai 2020.

Mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano ambao TIP imeupata kutoka kwa viongozi wa dini, wasaidizi wa kisheria na idara mbalimbali za serikali wilayani humo.

Kwa mujibu wa Afisa Ufuatiliaji na Tathmini, Respectson Akyoo na Afisa Mradi wa Boresha, Hamisi Kibayasi, kesi 32 zimeshughulikiwa na kufikia mwisho, huku ufuatiliaji ukiendelea kwa nyingine zaidi ya 70.

“Tumeshirikiana na wadau wetu kuibua kesi hizo katika kata 18 zinazoangaziwa na Mradi wa Boresha katika wilaya ya Kwimba yenye kata 30,” amesema Akyoo katika mazungumzo na waandishi wa habari wilayani Kwimba, hivi karibuni.

Maofisa wa Mradi wa Boresha wakizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya watoto wilayani Kwimba

Amesema kata hizo 18 ziliteuliwa na TIP kufanyiwa utafiti kutokana na kuwa na rekodi ya matukio mengi ya ukatili, hasa wa kingono kwa watoto na wa kimwili unaohusisha mashambulio kwa wanawake.

Akyoo amefafanua kuwa baadhi ya kesi za ukatili wa kingono kwa watoto zilizoibuliwa zinahusisha wanafunzi wa kike waliotoroshwa na kupewa ujauzito wilayani Kwimba.

Naye Kibayasi amefafanua kuwa katika utafiti huo, TIP imeekeza nguvu kubwa katika kufuatilia vitendo vya ukatili wa kingono kwa watoto kwa kuwa imebainika vinachangia maambukizi ya virusi vya Ukimwi na kukatisha masomo kwa watoto katika jamii.

Kibayasi amesema kabla ya kuanza utafiti huo, TIP kupitia Mradi wa Boresha ilitoa mafunzo elekezi kwa viongozi wa dini, wasaidizi wa kisheria na wakuu wa idara mbalimbali za serikali kuwajengea uwezo wa kuelimisha jamii madhara ya vitendo vya ukatili.

Mkurugenzi wa Wasaidizi wa Kisheria, Sagalani na Mchungaji Mathias Mleka wa AICT Ngudu, Kwimba wamesema TIP imewapatia mafunzo ambayo yanawasaidia kuelimisha wananchi madhara ya vitendo vya ukatili ukiwamo wa kingono kwa watoto katika jamii.

“Tumegundua kwamba watoto wamekuwa wakifanyiwa ukatili wa kingono katika sherehe na michezo ya ngoma… tunashukuru mafunzo tuliyopewa na TIP tunaendelea kuyasambaza na mwitikio wa jamii ni mkubwa,” amesema Mchungaji Mleka.

Hata hivyo, viongozi hao wamesema juhudi za kupambana na vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake wilayani Kwimba zinakabiliwa na vikwazo mbalimbali ikiwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kutokuwa tayari kufichua matukio hayo.

“Vikwazo vingine ni wahanga na familia zao kutotoa ushirikiano wa kutosha kwenye vyombo vya kisheria dhidi ya watuhumiwa wa vitendo hivyo na uhasama unaojengwa na watuhumiwa dhidi ya wafichuaji wa uhalifu huo,” ameongeza Sagalani.

Vikwazo vingine, kwa mujibu wa msaidizi huyo wa kisheria, ni baadhi ya viongozi wa vitongoji, mitaa na vijiji kugoma kutoa barua za kuwatambulisha wahanga wa ukatili kwenye vituo vya polisi, hali ambayo wakati mwingine husababisha polisi kukataa kuwapokea wahanga wa vitendo vya ukatili.

“Pia wanajamii wengi wamekuwa wakiogopa kuripoti polisi vitendo vya ukatili kwa hofu ya kushikiliwa na kuunganishwa kwenye orodha ya mashahidi wa matukio hayo. Kingine, tumebaini wanajamii wengi wana uelewa mdogo kuhusu matumizi ya Fomu Namba Tatu ya Polisi (PF3) kama kiambatanisho muhimu cha ushahidi,” ameongeza.

Kutokana na hali hiyo, Sagalani amesema elimu ya umuhimu na faida za matumizi ya fomu hiyo inahitajika kwa wananchi na viongozi wa serikali za mitaa, vitongoji na vijiji.

“Vilevile jamii ielimishwe faida za kujitokeza kutoa ushahidi na maafisa wa mashirika ya kupinga vitendo vya ukatili wapewe vyombo vya usafiri utakaowawezesha kufika maeneo ya matukio kwa wakati,” ameongeza

Mradi wa Boresha unatekelezwa chini ya Ushirikiano wa Kiimani Tanzania TIP unaoundwa na taasisi nne za kidini ambazo ni Baraza la Wakristo Tanzania (CCT), Baraza la Kitaifa la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Baraza la Maaskofu Wakatoliki Tanzania (TEC) na Ofisi ya Mufti wa Zanzibar (MoZ).

Kwa mujibu wa Akyoo, maono ya TIP ni kutengeneza mtandao thabiti wa kiimani unaochangia uwepo wa jamii ya Kitanzania yenye afya na kizazi kisicho na Ukimwii.

(Imeandikwa na Christopher Gamaina, Kwimba)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages