MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amezitaka taasisi
za kifedha nchini kuongeza mikopo kwa wakulima kuwawezesha kuongeza
uzalishaji, hivyo kukuza pato lao na taifa kwa jumla.
Samia ametoa rai hiyo jana wakati wa uzinduzi wa Maonesho ya
28 Nanenane yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Nyakabindi wilayani Bariadi,
Simiyu na kuongeza kuwa katika kipindi kilichopita utoaji wa mikopo kwa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi ulikuwa asilimia tisa.
Aidha, Makamu huyo wa Rais amewataka watafiti wa mbegu bora
kuweka wazi tafiti hizo kwa maafisa ugani kwa ajili ya kuzifikisha kwa wakulima
ili kuchochea uzalishaji wa mazao.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (katikati) akisikiliza maelezo kutoka kwa mtaalamu katika mojawapo ya mabanda ya Maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabidi |
Akizindua jengo la Wizara ya Kilimo katika viwanja hivyo vya
maonesho, lililogharimu shilingi milioni 400, Samia amewataka wasimamizi husika
kuhakikisha kuwa linatumika katika kuelimisha walengwa.
Awali, akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Kilimo,
Japheth Hasunga, amesema wizara hiyo imejipanga kuimarisha upatikanaji wa
malighafi kwenye viwanda vya ndani, pembejeo za kilimo, viuadudu na mbolea kwa
bei nafuu.
Waziri Hasunga amesema jengo hilo litatumika mwaka mzima
kuhamasisha shughuli za kilimo, mifugo na uvuvi, huku akiwasisitiza wananchi
kujitokeza kupata elimu itakayowasaidia kuongeza tija katika uzalishaji wa
mazao.
“Jengo hili na majengo mengine ya kilimo yatatumika pia kuelimisha
wananchi juu ya elimu ya lishe kwa lengo la kukabiliana na udumavu wa akili kwa
watoto wenye umri chini ya miaka mitano. Jumla ya watoto milioni tatu wana
udumavu wa akili… mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula ndio yenye idadi
kubwa ya watoto wenye tatizo hilo,” amesema.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan (katikati) akiendelea kutembelea mabanda ya bidhaa katika Maonesho ya Nanenane kwenye viwanja vya Nyakabindi |
Maonesho ya Nanenane yanafanyika kitaifa mkoani Simiyu kwa miaka mitatu mfululizo ambapo kaulimbiu ya mwaka huu inasema “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Chagua Viongozi Bora 2020”.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment