NEWS

Sunday 6 September 2020

Mamia washiriki mashindano ya Serengeti Migration Marathon


MASHINDANO ya Kimataifa ya Serengeti Migration Marathon yamefanyika kwa ufanisi leo Septemba 6, 2020 mjini Mugumu katika wilaya ya Serengeti mkoani Mara na kuhudhuriwa na mamia ya wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania.

 

Tanzania imeongoza kwa idadi kubwa ya wadau na wanariadha waliohudhuria na kushiriki mashindano hayo ikifuatiwa na nchi za Kenya na Ufaransa.

 

Mashindano hayo yamehusisha wanaume na wanawake katika mbio za kilomita 21.1, 10.1 na 5.2 ambapo washindi wamezawadiwa medali na fedha taslimu.

 

Mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21.1 kwa kila upande (wanaume na wanawake) amezawadiwa Sh 500,000, wa pili (Sh 350,000) na wa tatu (Sh 200,000).

 

Kwa upande wa mbio za kilomita 10.1, mshindi wa kwanza kwa kila upande amezawadiwa Sh 130,00, wa pili (Sh 100,000) na wa tatu (Sh 70,000), huku mshindi wa kwanza wa kilomita 5.2 akizawadiwa Sh 50,000, wa pili (Sh 40,000) na wa tatu (Sh 30,000).

Mmoja wa wanariadha walioshiriki mashindano hayo


Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, amepongeza waandaaji na washiriki wa mashindano hayo na kuahidi kuwa serikali ya mkoa huo itaanza kuchangia juhudi za kufanikisha mashindano ya mwakani.

Mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga (wa tatu kushoto) aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima kwenye Mashindano ya Kimataifa ya Serengeti Migration Marathon wilayani Serengeti leo Septemba 6, 2020. Wa pili kutoka kushusho ni Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nordin Babu

 

Mashindano hayo ya Serengeti Migration Marathon yameandaliwa na taasisi ya SETCO kupitia wakala wake wa michezo - Serengeti Tourism Sports Agency – SETSA.

 

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Samwel Nyankogoti, lengo kuu la mashindano hayo ni kuhamasisha uhifadhi na kutangaza utalii, hasa kwenye maeneo ya Magharibi mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (mkoani Mara) na Bonde la Mto Mara unaomwaga maji katika Ziwa Victoria.

 

Nyankogoti anayeshirikiana na Geoffrey Werema kuandaa mashindano hayo ametaja malengo mengine kuwa ni kufungua fursa za kiuchumi kwa wakazi wa maneo yaliyo jirani na hifadhi hiyo, mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo na eneo la Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori (Ikona WMA).

 

Pia kukuza vipaji vya wanariadha, hasa wanaotoka maeneo ya wilaya ya Serengeti na mkoa wa Mara kwa jumla, kuongeza idadi ya wageni/watalii wa ndani na wa nje wanauzuru katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti, eneo la Ikona WMA na vituo vya utalii wa kiutamaduni vilivyopo jirani.

 

Nyankogoti ametaja lengo jingine la mashindano hayo ya Serengeti Marathon kuwa ni kuchangia katika mapambano dhidi ya ujangili, hasa kwenye maeneo ya Ikona WMA, mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo, lakini pia katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

“Lengo jingine la mashindano hayo ni kuleta hamasa kwa wananchi kujenga tabia ya kupenda mazoezi, hasa kukimbia ili kulinda afya zao na kuepuka magonjwa yasio ya kuambukizwa,” ameongeza Nyankogoti.

 

Kesho Septemba 7, 2020 mashindano mengine maarumu ya riadha yanayolenga kupiga vita uwindaji haramu yatafanyika Fort Ikoma jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti chini ya uratibu wa taasisi ya SETCO.

 

Wadhamini wakuu wa mashindano hayo ni Bia ya Serengeti Larger ambao wameungana na wadau wengine wakiwamo Frankfurt Zoological Society (FZS), Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Ikona WMA, Grumeti Reserves, Serikali ya Mkoa wa Mara, Wilaya ya Serengeti na Mara Online kushuhudia burudani hiyo.

 (Imeandikwa na Christopher Gamaina, Serengeti)No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages