NEWS

Monday, 26 January 2026

DC Tarime awataka wakandarasi kuweka wazi BOQ za miradi



Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele.

Na Mwandishi Wetu
Tarime
-------------

Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Meja Edward Gowele, amewataka wakandarasi kuhakikisha wanaweka wazi Makadirio ya Gharama za Ujenzi (BOQ) na michoro ya miradi wanayopewa kuitekeleza.

DC Gowele alitoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata ya Matongo wilayani Tarime, wiki iliyopita.

Ni baada ya Mwenyekiti wa Serikali ya KIjiji cha Mjini Kati, Saroche, kumwambia kwamba ofisi yake haikuoneshwa BOQ na michoro ya ujenzi wa miundombinu ya shule unaoendelea kijijini hapo.

“Natoa maelekezo kwa wakandarasi, BOQ siyo siri, michoro ya ujenzi siyo siri, wanaosimamia ujenzi wapewe waone na wao wajiridhishe, hakuna sababu ya kuwanyima kwa sababu ni sehemu ya utekelezaji wa mradi.

“Kama mkandarasi, mhandisi na wananchi watakuwa na BOQ itasaidia kwa ufuatiliaji. Tunahitaji kushirikiana ili miradi itekelezeke kwa viwango. Miradi hii ni ya jamii, wana haki ya kujua kinachoendelea,” alisisitiza na kuongeza:

“Kwa hiyo, kuanzia sasa kamati ya ujenzi ipewe BOQ na michoro. Tunahitaji mahusiano mazuri kati ya mkandarasi, kamati za ujenzi na serikali za vijiji ili kuepusha mivutano kwenye utekelezaji wa miradi inayoenda kuleta tija kwa jamii.”

Sambamba na hilo, DC Gowele alimwagiza mkandarasi anayetekeleza mradi huo kurekebisha mapungufu yote yaliyoonekana kabla ya kuendelea na ujenzi na kuukabidhi.

Aidha, aliiagiza Idara ya Ujenzi ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kusimamia kwa ukaribu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya wananchi ili inapokabidhiwa isiwe na changamoto. “TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) nanyi piteni kuangalia,” alielekeza.

Chanzo : Gazeti la Sauti ya Mara 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages