NEWS

Saturday 12 September 2020

Mara Day, maonesho kilimo Butiama vipaishe uchumi Mara - Malima

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima akizungumza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mara yanayofanyika sambamba na maonesho ya kilimo kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama, jana.

 

WAKAZI wa mkoa wa Mara wamehimizwa kutumia maadhimisho ya Siku ya Mara na maonesho ya kilimo yanayoendelea katika viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama kujifunza teknolojia na kanuni bora za kilimo, lakini pia kuongeza ari ya kutunza mazingira yanayowazunguka na ikolojia ya Mto Mara.

 

Rai hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima wakati akifungua maadhimisho na maonesho hayo, jana Septemba 12, 2020.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima (wa tatu kushoto) akioneshwa mazao darasa katika maadhimisho ya Siku ya Mara yanayofanyika sambamba na maonesho ya kilimo kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama, jana. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Anarose Nyamubi.

 

“Maonesho haya yana umuhimu wa pekee katika mkoa wetu wa Mara, ninawaomba wananchi tuyatumie kujifunza kanuni bora za kilimo ili kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.

 

“Tunakumbushwa pia kutunza mazingira na ikolojia ya Mto Mara… ninataka maonesho haya yawe kichocheo cha kiuchumi na kijamii mkoani kwetu,” amesisitiza Malima.

Mwananchi akiangalia mkungu wa ndizi katika maadhimisho ya Siku ya Mara yanayofanyika sambamba na maonesho ya kilimo kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama, jana.

 

Amewashukuru wadau mbalimbali waliojitokeza kushiriki maadhimisho hayo kwa kujenga mabanda ya maonesho ya bidhaa zao wakiwamo kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI), Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, WWF, Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria na Ofisi ya Maji Bonde la Mto Mara.

 

Aidha, mkuu huyo wa mkoa amemshukuru mjane wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria Nyerere kwa kukubali viwanja vya maonesho hayo ya kilimo kupewa jina lake.

 

Pamoja na viongozi wengine, wakuu wa wilaya waliohudhuria ufunguzi wa maadhimisho hayo na wilaya zao zikiwa kwenye mabano ni Anarose Nyamubi (Butiama), Nordin Babu (Serengeti), Lydia Bupilipili (Bunda), Simon Odunga (Rorya) na Vincent Naano (Musoma).

Kikundi cha ngoma ya kiasili ya kabila la Wazanaki ikitumbuiza wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Siku ya Mara yanayofanyika sambamba na maonesho ya kilimo kwenye viwanja vya Mama Maria Nyerere wilayani Butiama, jana.

 

Maadhimisho hayo ya Siku ya Mara yanayofanyika sambamba na maonesho ya kilimo yameanza Septemba 12 na yatafikia kilele chake Septemba 15, 2020.

 

(Habari na picha zote na Christopher Gamaina, Butiama)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages