NEWS

Friday 11 September 2020

RUWASA kupanua huduma ya maji ya bomba Simiyu

Meneja wa RUWASA, Mhandisi Mariam Majala akionesha mambomba ya maji

UPATIKANAJI wa huduma ya maji safi na salama mkoani Simiyu unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 51 mwaka 2019 hadi  asilimia 57.4 ifikapo 0ktoba 2020 kupitia mradi wa lipa kulingana na matokeo (PF4R ), hivyo kuwezesha wananchi kupata huduma hiyo kwa uhakika na urahisi.

 

Pia kutakuwepo na ongezeko la ajira kwa wananchi kupitia mradi wa usambazazji wa mabomba katika miradi 23 itakayotekelezwa.

 

Hayo yamesemwa na Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Mhandisi Mariam Majala, wakati wa makabidhiano ya mabomba yatakayotumika kutekeleza miradi ya mji mkoani Simiyu, yaliyofanyika katika ofisi za RUWASA mjini Bariadi, leo Septemba 11, 2020.

 

Mhandisi Majala amesema mpaka sasa wamepokea asilimia 70 ya mabomba ya maji yenye thamani ya shilingi milioni 823 yatakayotumika kutekeleza miradi 23 katika mkoa mzima, huku asilimia 30 ya mabomba iliyobaki ikitarajiwa kuwasili wakati wowote kuanzia sasa.

 

“Hali ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa sasa sio mbaya na ninawahakikishia wananchi ongezeko kubwa la huduma hiyo," amesema Mhandisi Majala.

Meneja wa RUWASA, Mhandisi Mariam Majala (kushoto) akimwonesha Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga (kulia) mabomba ya maji

 

Awali, akikagua mabomba hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga, amewataka wananchi kushiriki kwenye mradi huo kwa kutunza miundombinu ya maji ili lengo la ongezeko hilo walilokusudia liweze kufikiwa, huku akiipongeza bodi ya ununuzi kwa kazi nzuri iliyofanyika.

 

"Niwatake wananchi wa mkoa huu ( Simiyu) kuitunza miundombinu ya maji inayotekelezwa na serikali ili iweze kudumu na kuwanufaisha wote kama ilivyokusudiwa," amesema Mmbaga.

 

Kwa upande wake, mjumbe wa bodi ununuzi, Ekwabi Mujungu, ameomba kazi ifanyike kama ilivyopagwa ili thamani ya fedha ionekane.

 

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages