NEWS

Tuesday 29 September 2020

RPC Mkonda: Polisi walifanyiwa fujo msafara wa Lissu Nyamongo

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi TarimeRorya, ACP William Mkonda.

KAMANDA wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi TarimeRorya, William Mkonda amesema kilichosababisha jeshi hilo kutumia mabomu ya machozi kutawanya wananchi katika msafara wa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tundu Lissu (Chadema), ni kitendo cha baadhi ya watu waliojitokeza kwenye msafara huo kuwafanyia fujo askari.

 

Katika taarifa yake ya ufafanuzi, Kamanda Mkonda amesema hali hiyo imetokea jana eneo la Nyamogo, Tarime Vijijini wakati Lissu alipoanza kusalimia wananchi waliojitokeza barabarani kushuhudia msafara wake wa kuelekea mkoani Arusha.

 

“Wakati anaanza kusalimia wananchi, gafla kundi la wafuasi wasiojulikana ni chama gani walianza kurushia askari (polisi) mawe hali iliyowasababisha kurusha mabomu kutawanya wananchi katika msafara huo. Watuhumiwa wanne tumewakamata, tunaendelea nao kwa mahojiano,” amesema kamanda huyo.

Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chadema, Tundu Lissu (aliyekaa juu ya gari) aliposimama kusalimia wananchi.

Lissu alifika Tarime Septemba 27, mwaka huu ambapo alihutubia mikutano mikubwa ya kampeni katika mji mdogo wa Sirari (jimbo la Tarime Vijijini), kisha mjini Tarime (jimbo la Tarime Mjini).

 

Ratiba yake, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ilikuwa kuondoka Septemba 28, mwaka huu asubuhi kwenda Arusha kupitia Serengeti.

 

“Polisi walienda kumsindikiza [Lissu], alitakiwa kuondoka Tarime mjini kupitia Nyamgwa na Mto Mara, lakini akazungukia Borega, Muriba kwenda Nyamongo,” amesema Kamanda Mkonda na kuendelea:

 

“Kimsingi Septemba 28 hakuwa na ratiba yoyote ndani ya Tarime Mjini na Tarime Vijijini, kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Alitakiwa kwenda moja kwa moja Arusha, lakini alisimama Muriba akasalimia wananchi, akasimama Nyamwaga… alipofika Kwinogo – Nyamongo akasimama.”

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Vijijini kwa tiketi ya Chadema, John Heche akizungumza katika mkutano wa kampeni siku mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama hicho, Tundu Lissu alipowasili jimboni humo.

 

Kutokana na hali iliyojitokeza, Kamanda Mkonda ametoa mwito kwa wagombea wote kufanya kampeni kwa kufuata maelekezo ya NEC ili kuepusha migongano kati ya chama na chama - ambayo zao lake ni uvunjifu wa amani.

 

“Pia natoa wito kwa wananchi kujiepusha na mihemko ya kisiasa inayosababisha uvunjifu wa amani. [Polisi] tutaendelea kusimamia amani wakati wote katika kipindi hiki cha kampeni za kuelekea upigaji kura na utangazaji wa matokeo ili kuwe na utulivu na amani, hatutamwonea haya atakayevunja amani,” ameongeza kamanda huyo wa polisi.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages