NEWS

Thursday 10 September 2020

World Vision Tanzania inavyokabili malaria Itilima

Kaimu Meneja wa Kanda ya Nzega kutoka World Vision Tanzania, Nyamoko George ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Kanadi, akizungumza wakati wa hafla ya ugawaji vyandarua wilayani Itilima

 

UGONJWA wa malaria bado unatajwa kuendelea kusumbua zaidi watoto umri wa chini ya miaka mitano wilayani Itilima, Simiyu.

 

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Dkt Anold Musiba, alipotoa taarifa ya hali ya malaria wilayani humo wakati wa ugawaji vyandarua vilivyotolewa na shirika lisilo la kiserikali la World Vision Tanzania, tukio lililofanyika katika kata ya Chinamili, jana Septemba 9, 2020.

 

Dkt Musiba amesema kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017, wagonjwa wa malaria wa nje (OPD) walikuwa 9,764, kati yao, watoto 4,159 sawa na asilimia 43 ambao wapo chini ya umri wa miaka mitano, mwaka 2018 walikuwa 6,209 wakiwamo watoto 2,460 sawa na asilimia 40 wenye umri chini ya umri wa miaka mitano.

 

Ameongeza kuwa kwa mwaka 2019 wagonjwa wa malaria wa nje walikuwa 6,432 wakiwamo watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano 2,693 sawa na asilimia 41 na kwa mwaka 2020 kuanzia Januari hadi Julai wagonjwa walikuwa 3,088 ambapo watoto chini ya umri wa miaka mitano walikuwa 1,449 sawa na asilimia 46.9.

 

Amesema kwa mwaka 2017 wagonjwa waliolazwa kutokana na kuugua malaria walikuwa 308 wakiwamo watoto chini ya umri wa miaka mitano 97 sawa na asilimia 31.7, mwaka 2018 walikuwa 245 wakiwamo watoto 106 sawa na asilimia 43.2, mwaka 2019 walikuwa 367 wakiwamo watoto 27 sawa na asilimia 34.6.

 

“Waliofariki kwa ugonjwa wa malaria kwa mwaka 2017 walikuwa 12, mwaka 2018 walikuwa watatu, 2019 walikuwa watano, kuanzia Januari hadi Julai kulikuwa na vifo sita na kiwango cha maambukizi kwa wilaya ya Itilima ni asilimia 5.1,” amesema Dkt Musiba.

Baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya ugawaji wa vyandarua vya kujikinga na ugonjwa wa malaria wilayani Itilima

 

Hata hivyo, amesema katika mapambano dhidi ya malaria, halmashauri imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kwa kutoa elimu/ kuhamasisha wananchi kufuata kanuni na njia bora za kujikinga na ugonjwa huo kwa kutumia vyandarua vyenye viuatilifu.

 

Pia kwa upuliziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye maeneo yenye mazalia ya mbu, kutoa tiba kinga kwa wajawazito na kusafisha maeneo ya makazi ili kuharibu mazalia ya mbu waenezao malaria.

 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, Philibert Kanyilizu, amewaomba wadau kuendelea kujitokeza kuunga juhudi za kutokomeza ugonjwa wa malaria.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Dkt Anold Musiba, akizungumza wakati wa hafla ya kugawa vyandarua kwa wananchi

 

Awali, akimkaribisha mgeni rasmi, Kaimu Meneja wa Kanda ya Nzega kutoka World Vision Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa Kanadi, Nyamoko George, amesema Sh milioni 38.676 zilizotolewa na wafadhili zimetumika kununua vyandarua vyenye viuatilifu vinavyodumu kwa muda mrefu vipatavyo 6,160 ambavyo vimegawiwa kwa watoto wafadhiliwa 3,431 na wasio fadhiliwa 2,729 kupitia mradi wa World Vision.

 

“Shirika la World Vision Tanzania linaungana na Serikali ya Awamu ya Tano katika juhudi za kupambana na kutokomeza ugonjwa wa malaria na tunaamini kwa vyandarua hivi 6,160 maambukizi ya malaria yatapungua kama si kuisha kabisa tukizingatia mpango mkakati wa wizara kupunguza kiwango cha maambukizi ya malaria kutoka asilimia saba hadi chini ya asilimia moja ifikapo mwkaa 2020 na kuitokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030,” amesema George.

 

Wakizungumza mara baada ya kukabidhiwa vyandarua vilivyotolewa na World Vision Tanzania, wazazi na watoto wamesema vitakuwa msaada mkubwa wa kukabiliana na ugonjwa wa malaria.

Kazi ya ugawaji vyandarua ikiandelea

 

“Chandarua kitanisaidia kujikinga na malaria, nitasoma vizuri, zamani nilikuwa naugua sana malaria maana nyumbani hatukuwa na chandarua, mbu walikuwa wakining'ata, sasa hivi malaria basi,” amesema Nkumba Masunga, mwanafunzi wa Shule ya Msingi Nanga ‘B’ ya wilayani Itilima.

hughuli ya ugawaji vyandarua vya kujikinga na malaria wilayani Itilima


“Awali tulikuwa tunawapeleka watoto hospitali ukifika unaambiwa ni malaria unapewa dawa anatumia, mkirudi nyumbani anang'atwa na mbu tena mnarudi hospitali ugonjwa ni ule ule, tunawashukuru sana World Vision Tanzania kwa msaada huu utatusaidia kujiinua kiuchumi, tutafanya kazi na kujiongezea kipata badala ya kutumia muda mwingi na gharama kujitIbu maralia,” amesema mmoja wa wazazi, Ngolo Masengo.

 

(Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Itilima)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages