
MNEC Gachuma (katikati), Mbunge Mary (kulia) na wadau wengine wakifurahia picha ya pamoja baada ya Sekondari ya Manga kuwatunuku tuzo, Agosti 13, 2026. Wa tatu kushoto ni Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Editha Lazaro Nakei.
Tarime
-------------
Shule ya Sekondari Manga iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, imetoa tuzo kwa wadau wake wa maendeleo, akiwemo mwanasiasa na mfanyabisahara maarufu Kanda ya Ziwa, Christopher Mwita Gachuma, ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama tawala - CCM.
Tuzo hizo zilitolewa kwa MNEC Gachuma na wadau wengine katika hafla iliyofanyika shuleni hapo Agosti 13, 2026, ikiwa ni kutambua mchango wao kwa maendeleo ya shule hiyo ambayo yenye mamia ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita.
Aidha, Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Editha Lazaro Nakei, alitumia fursa hiyo pia kutoa motisha ya fedha kwa walimu na wafanyakazi wasio walimu kwa kazi nzuri wanayofanya shuleni hapo.
“Hili jambo la tuzo kwa wadau wa maendeleo na kuwapatia walimu motisha mlilofanya katika shule yenu ni kubwa, hongereni sana,” alisema Mwenyekti wa Halmshauri ya Mji wa Tarime, Thobias Elias Ghati ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo kwa niaba ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete.

MNEC Gachuma (kushoto) akipokea tuzo yake kutoka kwa Mwenyekiti Thobias.
Mbali na MNEC Gachuma, wadau wengine waliotunukiwa tuzo hizo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi na Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Chacha Range.
Wengine ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Matera Newland Chacha na Mkurugenzi wa Mara Online, Jacob Mugini ambaye ni mwandishi wa habari kitaaluma.

Mkurugenzi wa Mara Online, Jacob Mugini (kushoto), akikabidhiwa tuzo yake. (Picha zote na Mara Online News)
Uongozi wa shule hiyo chini ya Mwalimu Nakei, ulikabidhi pia zawadi ya laptop kwa mwanfunzi bora aliyevunja rekodi ya kupata ufauku wa daraja la kwanza la alama nne katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Sita 2026, Deborah Musa Robert.
Akizungumza katika hafla hiyo, Gachuma alieleza kufurahishwa na maendeleo ya shule hiyo na kuahidi kuendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine kuiboreshea mazingira ya kujifunzia na kufundishia.
Akitoa salamu za Mbunge Ghati Zephania Chomete katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Thobias, alisema mbunge huyo atatoa saruji mifuko 50 kuchangia ukarabati wa baadhi ya miundoimbinu ya shule hiyo.
MNEC Gachuma aliahidi kumsindikiza kwa kutoa saruji mifuko 50, huku Mkurugeni wa Kampuni ya Soya One Limited, Chacha Marwa Gesora naye akiahidi kuchangia saruji mifuko 40 na Maswi akiahidi kutoa maofali ya ‘block’ 500.
Mkurugenzi wa Soya One alimwakilisha Katibu Mkuu Maswi katika hafla hiyo ambayo ilihudhuriwa pia na Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Mary Daniel Surati.
Mbunge huyo kijana alisema mwanafunzi bora aliyefanya vizuri katika shule hiyo, Deborah, atajiunga na kundi jingine la wanafunzi ambao wamefanya vizuri katika mitihani yao kutoka wilayani Serengeti kufanya ziara katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania jijini Dodoma kupitia programu yake ya Samia Uthubutu Award.
Wakati wa ziara hiyo, mwanafuzi huyo atafuatana na mwalimu mmoja wa kike kutoka Shule ya Sekondari Manga, alisema Mbunge Mary.
Manga ni moja ya shule za serikali zenye wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita katika wilaya ya Tarime mkoani Mara.
Shule hiyo inapokea wanafunzi wa kike wa kidato cha tano na cha sita (high school) kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Matokeo ya ufaulu kwa wanafunzi wanaomaliza kidato cha nne na cha sita katika shule hiyo yanaripotiwa kuwa mazuri.
Hata hivyo, shule hiyo bado inakabiliwa na ukosefu wa jengo la maktaba, nyumba za walimu na uchakavu wa baadhi ya vyumba vya madarasa.
Hivyo, Mkuu wa Shule, Mwalimu Nakei, aliiomba Halmashauri ya Wilaya ya Tarime na wadau wengine kujitokeza kusaidia kutatua changamoto hizo.
Maafisa elimu kutoka halmashauri ya wilaya hiyo ni miongoni mwa wageni walioshiriki katika hafla hiyo ambayo ilifanyika katika ukumbi wa shule hiyo.
No comments:
Post a Comment