NEWS

Monday, 12 October 2020

Alliance Ginnery yajenga VETA, yaikabidhi serikalini Simiyu

Jengo la chuo cha VETA Kasoli kilichojengwa na Kampuni ya Alliance Ginnery.

 

MKURUGENZI Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Dkt Maduhu Kazi amewataka wawekezaji nchini kuangalia namna ya kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao. 

Aidha, Dkt Kazi amesema TIC itakuwa mstari wa mbele katika kutatua changamoto za wawekezaji kwa wakati na kwamba kipaumbele chake ni kuongeza ufanisi katika kuwasaidia wawekezaji hususan katika kupata vibali kwa lengo la kuwafikia wawekezaji wadogo ambao asilimia kubwa ni wazawa na amewataka kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hiyo.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt Maduhu Kazi (wa pili kushoto - mwenye tai) na viongozi wengine katika chuo cha veta Kasoli juzi.


Dkt Kazi ameyasema hayo Oktoba 9, 2020 wakati makabidhiano ya chuo mafunzo ya ufundi (VETA) Kasoli kilichopo kijiji cha Kasoli wilayani Bariadi, Simiyu - kilichojengwa na mwekezaji Alliance Ginnery Limited na kukabidhiwa kwa serikali na Mkurugenzi Mtendaji wa TIC kwa niaba ya kampuni hiyo ambapo kimepokewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kwa niaba ya wananchi. 

"Naipongeza na kuishukuru kampuni ya Alliance Ginnery kwa kujenga chuo cha mafunzo ya ufundi (VETA), nitoe wito kwa wawekezaji wengine kuona umuhimu wa kuwafikia wananchi walio katika maeneo yao, naahidi TIC itahakikisha inakuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili wawekezaji," amesema Dkt Kazi na kuongeza:

“TIC inashirikiana na serikali ngazi ya mikoa na tumejielekeza zaidi kuongeza ufanisi katika shughuli zetu za kuwasaidia wawekezaji masuala ya vibali kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika. Pia tumejipanga kuwafikia wawekezaji wadogo Watanzania maana baada ya tathmini tumeona eneo hilo kuna mapungufu - wengi wanadhani sisi tunahusika na wawekezaji wa kigeni tu,” ameongeza  Dkt Kazi.


Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Dkt Maduhu Kazi (wa tatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (wa tatu kushoto) na viongozi wengine wakati wa ukataji utepe katika chuo cha VETA Kasoli juzi.

Mara baada ya kupokea chuo hicho, Mtaka ametoa wito kwa wazazi na walezi kuwapunguzia kazi wanafunzi wa darasa la nne, kidato cha pili na cha nne wanaoelekea kufanya mitihani ya taifa Novemba mwaka huu ili waweze kujipatia muda mwingi wa kujisomea kujiandaa na mitihani hiyo.

“Darasa la saba wameshafanya mtihani wao, watoto wa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne waendelee kufanya maandalizi, wazazi na walezi wapunguzieni kazi watoto wote walio kwenye madarasa ya mitihani na wakiwa nyumbani wafanye majadiliano ya pamoja, mkitaka kutoka kwenye umaskini somesheni watoto,” amesisitiza Mtaka na kuongeza:

"Nitoe onya kwa  wazazi na walezi wenye nia ya kuwaozesha wanafunzi wa kike waliohitimu elimu ya msingi hawa ni mali ya serikali, tukikubaini hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yako. Nitoe wito tena kwa jamii yote kuwa walinzi wa watoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.”


Viongozi mbalimbali ndani ya chuo cha VETA Kasoli juzi.

Mbali na hilo, Mtaka ameishukuru Kampuni ya Allience Ginnery kwa kujenga chuo cha VETA Kasoli na kutoa wito kwa wasichana na wanawake kijijini hapo kujitokeza kupata mafunzo ya ushonaji bila malipo katika kipindi cha Oktoba hadi Desemba mwaka huu kabla ya kuanza kwa mafunzo mengine mwakani kwa mtaala wa serikali, ambapo ameahidi kukipatia chuo hicho msaada wa vyerehani 25.


Viongozi wakikagua mradi wa maji katika chuo cha VETA Kasoli juzi.

Boaz Ogolla ambaye ni Meneja Mkuu wa Alliance Ginnery Limited, amesema kampuni hiyo inajihusisha na maendeleo ya jamii katika sekta ya elimu, afya na maji na kuongeza kuwa wao ni sehemu ya jamii, hivyo ni wajibu wao kufanya shughuli za kijamii ikiwa ni sehemu ya maelekezo ya TIC wanayopewa wawekezaji wote.

Pamoja na mafunzo ya ufundi, Ogolla amesema mipango ya baadaye ya kampuni hiyo ni kuongeza darasa moja la wakulima kwa lengo la kutoa warsha na mafunzo kwa wakulima waweze kulima kwa tija ili kampuni hiyo ipate malighafi bora kwa ajili ya kiwanda cha kuchambua pamba.


Viongozi wakikagua mojawapo ya vyumba vya majengo ya chuo cha VETA Kasoli juzi.

"Sisi kama kampuni tunajiona kama sehemu ya jamii ni wajibu wetu, mipango bado ni mingi, tuna mpango wa kupanua kozi mbalimbali mfano za udereva ili watoto wetu wasiende mbali kutafuta ujuzi na hii itasaidia kuwapunguzia gharama wazazi/walezi,” amesema Ogolla na kuongeza: 

“Tunampango wa kuongeza darasa moja kwa wakulima, sisi tunashughulika na wakulima na wanaolimi pamba na kutuuzia hatua inayotuwezesha kuendesha kiwanda chetu. Siku za nyuma tulijikita kwenye afya, maji, elimu ya msingi na sekondari, sasa tumeona haja ya kujenga chuo cha ufundi ili wanafunzi watakaoshindwa kuendelea na masomo wapate mafunzo ya ufundi waweze kujitegemea.”


Waigizaji wa kikundi cha Futuhi wakitoa burudani wakati wa makabidhiano ya chuo cha VETA Kasoli juzi.

Naye mkazi wa kijiji cha Kasoli, Shamsa Abdallah ameishukuru kampuni ya Alliance Ginnery kwa kuwajengea chuo cha VETA akisema anaamini kitawasadia kwenye mafunzo ya ushonaji na yanayohusiana na kilimo yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Viongozi mbalimbali akiwemo Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na wananchi wakiburudika mara baada ya makabishiano ya chuo cha VETA Kasoli kilichojengwa na Kampuni ya Alliance Ginnery juzi.

 

Kampuni ya Alliance Ginnery Limited imejenga majengo ya chuo hicho kwa gharama ya Sh milioni 180, mbali na gharama hizo, pia shughuli nyingine zimefanywa ikiwa ni pamoja na kuchimba kisima cha maji chenye uwezo wa kutoa lita 5,000 kwa saa na kuweka vifaa kama vyerehani, majiko ya gesi na vifaa mbalimbali vya upishi, kujifunzia uashi na useremala, meza na viti vya ofisi, ambapo zimetumika Sh zaidi ya milioni 180.

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages