NEWS

Monday 12 October 2020

DC aingilia kati mgogoro mgodi wa Burumbaka

Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akizungumza na wadau katika mgodi wa dhahabu wa Burumbaka

 

SERIKALI imeutaka mgodi wa dhahabu wa Burumbaka uliopo kata Gasuma wilayani Bariadi, Simiyu kumaliza mgogoro uliopo la sivyo itaufunga.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alipofanya ziara mgodini hapo kufuatia mgogoro uliotokea baada ya baadhi ya walioshindwa kutokubaliana na uongozi mpya.

Kiswaga amesema awali Afisa Madini aliteua kamati ya kusimamia madini isiyo ya kisheria, hivyo akaleta waraka ambao unataka kuwa na kikundi ambacho kipo kisheria hatua iliyosababisha kufanya utaratibu wa kupata viongozi kisheria.

"Kuna watu wanapenda vurugu ziendelee ili wajinufaishe wao na kuna taarifa za utoroshwaji wa madini usiku, tukiwakamata wanaohusika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao," amesema Kiswaga na kuongeza:

"Hizi virugu hazina afya kwenye uchumi na kama serikali itaona vurugu zinaendelea tutasimamisha shughuli za mgodi mpaka hapo hali itakapokuwa vizuri... hatutakubali kuona damu ya mtu inamwagika. Kikubwa hapa kwanza maslahi ya wananchi hususan wenye mashamba maana awali walikuwa wanalima hapa na kuvuna."

Mkuu huyo wa wilaya ameongeza kuwa tayari kuna majina ya watu wanaotajwa sana yakihusishwa na mgogoro huo, hivyo amemtaka Kaimu Afisa Madini kuhakikisha watu hao hawakanyagi mgodini hapo.

Mbali na hayo, Kiswaga amesema waliopewa zabuni ni wale ambao mashamba/makazi  yao yamegeuzwa mgodi na ambao ni wazawa, baadaye ikatokea sintofahamu kutokana na uwepo wa vikundi vilivyopo kwenye mgodi huo kuwa vingi.

"Vikundi vilivyopo ni vingi lakini kikundi cha wenye mashamba ndio kimetoa mwenyekiti na katibu msaidizi na hapa kinachoonekana kuna wale walioshindwa ndio wanataka kuhamasisha vurugu," amesema Kiswaga

Sehemu ya eneo la mgodi wa dhahabu wa Burumbaka.


Kwa upande wake, Kaimu Afisa Madini Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Oscar Kalowa amesema Oktoba 9, 2020 kulikuwa na kikao kilichoitishwa na mamlaka za mkoa kilichofanyika kwenye ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo kilichowahusisha wamiliki wa mashamba na vikundi vilivyoomba zabuni ya usimamizi wa rush (migodi midogo midogo) ya Burumbaka kwa lengo la kuwakutanisha pamoja wachimbaji ili kufanya shughuli ya usimamizi.

Mhandisi Kalowa ameongeza kuwa kikao kilikuwa shirikishi na mjadala ulifanyika kwa mafanikio na vikundi vilivyoshiriki ni kikundi cha wamiliki wa mashamba (Umoja Burumbaka), ubunifu, Burumbaka Wajasilismali na Umoja ni Nguvu ambapo kwa pamoja walijadiliana na hatimaye wakaweka uongozi ambao utasimamia Burumbaka rush.

Awali, baadhi ya wamiliki wa mashamba wamesema hawana imani na uongozi uliowekwa huku wengine wakidai kuwa baadhi ya viongozi waliochaguliwa sio waaminifu.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages