NEWS

Saturday 10 October 2020

Kembaki kuanzisha SACCOS ya mikopo bila riba Tarime Mjini

Mbombe ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Michael Kembaki akijinadi katika moja ya mikutano yake ya kampeni jimboni humo.

 

MGOMBEA ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Michael Kembaki ameahidi kuanzisha SACCOS ili kuwawezesha kiuchumi wajasiriamali wakiwemo wakulima wa ndizi na mazao mengine. 

“Nikipata ridhaa ya wananchi ya kuwa mbunge nitaanzisha SACCOS itakayoitwa Tarime SACCOS, ambayo itatoa mikpo ya mitambo ya kusindika mazao kama vile ndizi bila riba,” amesema Kembaki katika mkutano wake wa kampeni uliofanyikwa katani Turwa, juzi Ijumaa. 

Kembaki pia ameahidi kuanzisha viwanda vidigo vidogo ambavyo vitapanua wigo wa soko kwa mazao ya wakulima na ajira kwa vijana. 

Pia mgombea ubunge huyo ametaja vipaumbele vyake kuwa vitakuwa ni kuboresha huduma za jamii ikiwemo elimu, afya, maji na barabara katika jimbo la Tarime Mjini.

Kuhusu afya, ameahidi kujenga zahanati mbili katika kata ya Kenyamanyori na kuanzisha mpango mkakati wa kuboresha miundombinu ya shule za msingi na sekondari.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki akiomba kura kwa wananchi katika mkutano wa kampeni uliofanyika katani Turwa, juzi.

Kwa upande mwingine, Kembaki ameahidi kuwa akichaguliwa atasimamia ujenzi wa soko la kisasa la Tarime na kuhakikisha mji huo unapata huduma ya maji safi na salama kutoka Ziwa Victoria.

Mgombea huyo anaendelea na kampeni zake ikiwa ni pamoja na kupita mtaa kwa mtaa kuwaomba wananchi wa jimbo la Tarime Mjini kumchagua katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Mamia ya wananchi wakimshangilia mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kwa tiketi ya CCM, Michael Kembaki katika moja ya mikutano yake ya kampeni jimboni humo.


Hivi karibuni, uongozi wa CCM Wilaya ya Tarime umethibitisha kuimarisha kampeni za Kembaki katika jimbo hilo na hivyo kumeweka mgombea huyo katika nafasi nzuri ya ushindani. 

“Tayari tumemaliza kata zote na sasa hivi tunafanya marudio ya kampeni mtaa kwa mtaa na hali yetu ni nzuri,” Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Hamis Mkaruka amewaambia waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa wananchi waliozungumza na Mara Online News kwa nyakati tofauti juzi na jana, nyota ya Kembaki imeendelea kung’ara siku hadi siku katika kinyang’anyiro cha ubunge wa Tarime Mjini.

“Upepo wa Kembaki sasa hivi ni mzuri sana. Unajua huyu ni mgombea mnyenyekevu na aliyetulia, anafanya kampeni zake kwa staha bila kutukana mtu,” amesema Joseph Mwita, mkazi wa jimbo hilo.

Mgombea ubunge jimbo la Tarime Mjini kupitia CCM, Michael Kembaki akisalimia wazee katika senta ya Mogabiri katani Kenyamanyori alipokwenda kuomba kura, jana.

Jambo jingine linalotajwa kumbeba Kembaki katika kinyang’anyiro hicho ni kitendo chake cha kijitolea kushiriki katika shughuli za maendeleo jimboni humo hata baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

“Watu wanasema Kembaki ni mtu ambaye hakati tamaa na amekuwa akichangia shughuli za maendeo ya jimbo la Tarime Mjini. Tangu mwaka 2015 ameendelea kuchagia uboreshaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, hasa elimu katika jimbo letu,” amesema mkazi mwingine wa jimbo hilo, Hawa Kimito.

Katika kinyang’anyiro cha ubunge wa jimbo la Tarime Mjini, Kembaki anachuna na Esther Matiko wa Chadema anayetetea nafasi hiyo na Mary Nyagabona wa NCCR - Mageuzi.

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages