UZIO uliojengwa kwa ajili
ya kulinda faru katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori yanayopakana na vijiji
mbalimbali wilayani Serengeti, Mara umegeuka neema kwa wananchi.
“Mbali na kulinda faru,
uzio huo umekuwa na faida ya kuzuia tembo kuvamia na kuharibu mazao ya chakula
katika vijiji jirani,” Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile
alisema katika mazungumzo na Mara Online News, hivi karibuni.
Mwakipesile alitaja vijiji
vinavyonufaika na uzio huo kuwa ni Bonchugu, Kazi, Mbirikiri, Rwamchanga,
Miseke na Park Nyigoti.
Alisema awamu ya kwanza ya
uzio huo ulihusisha umbali wa kilomita zaidi ya 30 na kwamba baada ya kuona
hivyo, vijiji vingine vimeomba uzio kama huo kujengwa katika maeneo yao ili uwasaidie
pia kuzuia wanyamapori ambao wamekuwa wakivamia na kufanya uharibifu wa mazao
ya chakula.
“Tayari maandalizi ya
kuweka uzio awamu ya pili yanaendelea na sehemu kubwa ya wananchi wanatamani
uzio kwenye maeneo yao,” alisema Mwaki[pesile.
Meneja uhusiano huyo wa
Grumeti Fundi alitaja baadhi ya vijiji vitakavyonufaika na awamu ya pili ya
mradi huo wa uzio kuwa ni Nyichoka, Nyanungu na Makundusi.
Alisema mbali na tembo,
uzio huo utazuia wanyamapori wengine kama fisi kuingia katika mashamba au makazi ya wananchi.
Viongozi wa vijiji wanena
Viongozi wa vijiji ambako
uzio huo umepita wamekiri kuwa umesadia kuzuia tembo kuvamia na kuharibu mazao
ya chakula na biashara vijijini.
“Mfano katika kijiji cha
Bonchugu tembo hawakuharibu mashamba [msimu uliopita] na watu walivuna japo
shida ilikuwa ni hali ya hewa,” alisema Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bonchugu,
Rehema Lucas Mtani.
Mtani alisema hivi sasa
tembo hawapiti katika maeneo ambayo yamewekewa uzio. “Uzio unasadia kwa tembo
ila fisi bado,” alisema.
Mwenyekiti wa Serikali ya
Kijiji cha Nyanungu, Chacha Mwikwabe Mrimi alisema wananchi wake wanasubiri
awamu pili ya uzio huo kwa shauku kubwa.
“Sisi serikali ya kijiji
na mkutano mkuu wa kijiji tumepokea mradi huu wa uzio na kuupitisha na wananchi
wanasubiri uzio kwa hamu sana, maana wanaoathirika ni wananchi wakulima
wakaida,” alisema Mrimi.
Grumeti Fund yapunguza migogoro
ya binadamu, wanyamapori
Meneja Uhusiano,
Mwakipesile, alisema taasisi ya Grumeti Fund kwa kushirikiana na serikali kupitia
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na idara za wanyamapori
katika halmashauri za wilaya za Serengeti na Bunda zimekuwa vikifanya juhudi
mbalimbali kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyampori.
“Kwanza tulifanya utafiti
wa kubaini mapito na mwenendo wa tembo, kisha kwa kuhirikiana na TAWIRI
tukawafungia tembo kifaa maalumu (collar) cha kufuatilia mwenendo wao,”
alisema.
Ufutiliaji huo alisema
umekuwa ukisadia kuzuia tembo kabla hawajavamia mazao ya chakula au kuingia
kwenye makazi ya waanachi.
Lakini pia Grumeti Fund
kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na
Kikosi Kazi didhi ya Ujangili Bunda (KDU) zimeanzisha kikosi maalumu cha kuzuia
wanyamapori, hususan ambao wamekuwa wakivamia na kuharibu mazao ya wananchi.
“Lakini pia tumeanzisha
free number (namba ya simu ya kupiga bure) ambayo wananchi hupiga simu saa 24
kutoa taarifa ya uwepo wa tembo katika maeneo yao na kupata msaada wa
kuwafukuza kwa haraka,” alisema Mwakipesile.
Aidha, aliongeza kuwa
wameendelea kutoa elimu kuhusu wanyamapori waharibifu katika vijiji vya wilaya
za Serengeti na Bunda. ”Tunatoa elimu kupitia cinema, michezo, vikao na jarida
letu la Sauti ya Grumeti,” alifafanua.
No comments:
Post a Comment