NEWS

Monday 2 November 2020

Wahitimu Angel House Sekondari wadokezwa siri ya mafanikio

Wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Angel House wakitumbuiza wakati wa mamafali yao shuleni hapo, Ijumaa iliyopita.


WAHITIMU wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Angel House iliyopo Tarime mkoani Mara wamehimizwa kujikita katika nidhamu, bidii ya kusoma na kujiamini waweze kutimiza ndoto zao za mafanikio maishani.

 

Ushauri huo umetolewa na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Taasisi ya Mara Online, Mugini Jacob, katika sherehe za mahafali ya tisa ya wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo, Ijumaa Oktoba 31, 2020.

 

Taasisi ya Mara Online yenye makao makuu yake mjini Tarime, ndio inayomiliki gazeti hili [Sauti ya Mara] na blogu ya Mara Online News.

CEO wa Mara Online, Mugini Jacob (kushoto) na Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Angel House, Nyamchele Andrew wakipita katikati ya vijana wa skauti wa shule hiyo, ambapo Jacob alialikwa kuwa mgeni rasmi wa mahafali ya wahitimu wa kidato cha nne, Ijumaa iliyopita.

 

“Endeleeni kudumisha nidhamu yenu, kusoma na kufanya kazi kwa bidii, vitu hivi vitawafikisha mbali kimafanikio,” Jacob amewambia wahitimu hao 72 (wasichana 36 na wavulana 36).

 

Ameongeza kuwa bidii ya kusoma itawawezesha kufaulu vizuri mtihani wa taifa wa kuhitimu kidato cha nne utakaofanyika baadaye mwezi huu.

 

“Mkifaulu vizuri kwenye mtihani huo mtachaguliwa kuendelea na masomo ya juu, lakini pia mtawafurahisha wazazi na walezi wenu ambao wanatumia fedha nyingi kuwasomesha.

 

“Lakini pia mtakapomaliza mtihani na kurudi nyumbani kusubiri matokeo, jiepusheni na vitendo visivyofaa katika jamii na muwe na ujasiri wa kuzishinda changamoto zinazojitokeza mbele yenu. Amini katika kuweza, usiamini katika kushindwa,” alisema Jacob aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo.

Mgeni rasmi, Mugini Jacob (katikati), akihutubia wakati wa mahafali ya tisa ya wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Angel House. Waliokaa mbele kulia ni Makamu Mkuu wa Shule, Nyamchele Andrew na kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Grass Roots Tanzania linalomiliki shule hiyo.

 

CEO huyo wa Mara Online ametumia nafasi hiyo pia kuhimiza wazazi na walezi kuwa tayari kuwasikiliza na kuwasaidia watoto wao kwa hali na mali ili waweze kutimiza ndoto zao.

 

Aidha, amepongeza uongozi, walimu, wanafunzi na watumishi wote wa shule hiyo kwa ushirikiano na ubunifu wao ulioipaisha kitaaluma na kuiwezesha kushika nafasi za juu kwa ufaulu wa mitihani ngazi ya wilaya, mkoa na taifa.

 

Awali, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Angel House, Nyamchele Florence Andrew, amemweleza mgeni rasmi kwamba shule hiyo ina wanafunzi 316 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, walimu 23 na watumishi wengine 22, miradi ya ufugaji ng’ombe wa maziwa, nyuki na sungura.

Wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Angel House wakicheza kwa madaha wakati wa mahafali yao shuleni hapo, Ijumaa iliyopita.

 

Katika mahali hayo yaliyotumbuizwa na vikundi mbalimbali vya burudani vya wanafunzi, mgeni rasmi, Jacob, amepewa heshima ya kukabidhi zawadi na vyeti vya utambuzi kwa wanafunzi, walimu na wafanyakazi walioonesha utendaji bora zaidi kwenye vitengo vyao.

Mgeni rasmi, Mugini Jacob (katikati) akikabidhi cheti cha utambuzi kwa mmoja wa wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Angel House wakati wa mahafali ya tisa ya shule hiyo Ijumaa iliyopita. Kushoto ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Grass Roots Tanzania linalomiliki shule hiyo, Joseph Nyirah

 

Viongozi wengine waliohudhuria mahafali hayo ni pamoja na Mkuu wa Shule hiyo, Mwita Samson Marwa, Mwenyekiti wa Bodi ya Sekondari hiyo, Bernadina Nyambita na Joseph Nyiraha ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Grass Roots Tanzania linalomiliki shule hiyo na kituo cha kulea watoto yatima cha Angel wilayani hapa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Angel House, Bernadina Nyambita (aliyesimama) akizungumza katika mahafali ya tisa ya wahitimu wa kidato cha nne shuleni hapo, Ijumaa Iliyopita.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages