NEWS

Thursday 5 November 2020

Uzio wa faru kicheko kwa wanavijiji Serengeti

 

UZIO uliojengwa kwa ajili ya kulinda faru katika maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori yanayopakana na vijiji mbalimbali wilayani Serengeti, Mara umegeuka neema kwa wananchi.

 

“Mbali na kulinda faru, uzio huo umekuwa na faida ya kuzuia tembo kuvamia na kuharibu mazao ya chakula katika vijiji jirani,” Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile alisema katika mazungumzo na Mara Online News, hivi karibuni.

 

Mwakipesile alitaja vijiji vinavyonufaika na uzio huo kuwa ni Bonchugu, Kazi, Mbirikiri, Rwamchanga, Miseke na Park Nyigoti.

 

Alisema awamu ya kwanza ya uzio huo ulihusisha umbali wa kilomita zaidi ya 30 na kwamba baada ya kuona hivyo, vijiji vingine vimeomba uzio kama huo kujengwa katika maeneo yao ili uwasaidie pia kuzuia wanyamapori ambao wamekuwa wakivamia na kufanya uharibifu wa mazao ya chakula.

 

“Tayari maandalizi ya kuweka uzio awamu ya pili yanaendelea na sehemu kubwa ya wananchi wanatamani uzio kwenye maeneo yao,” alisema Mwaki[pesile.

 

Meneja uhusiano huyo wa Grumeti Fundi alitaja baadhi ya vijiji vitakavyonufaika na awamu ya pili ya mradi huo wa uzio kuwa ni Nyichoka, Nyanungu na Makundusi.

 

Alisema mbali na tembo, uzio huo utazuia wanyamapori wengine kama fisi kuingia katika  mashamba au makazi ya wananchi.

 

Viongozi wa vijiji wanena

 

Viongozi wa vijiji ambako uzio huo umepita wamekiri kuwa umesadia kuzuia tembo kuvamia na kuharibu mazao ya chakula na biashara vijijini.

 

“Mfano katika kijiji cha Bonchugu tembo hawakuharibu mashamba [msimu uliopita] na watu walivuna japo shida ilikuwa ni hali ya hewa,” alisema Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Bonchugu, Rehema Lucas Mtani.

 

Mtani alisema hivi sasa tembo hawapiti katika maeneo ambayo yamewekewa uzio. “Uzio unasadia kwa tembo ila fisi bado,” alisema.

 

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyanungu, Chacha Mwikwabe Mrimi alisema wananchi wake wanasubiri awamu pili ya uzio huo kwa shauku kubwa.

 

“Sisi serikali ya kijiji na mkutano mkuu wa kijiji tumepokea mradi huu wa uzio na kuupitisha na wananchi wanasubiri uzio kwa hamu sana, maana wanaoathirika ni wananchi wakulima wakaida,” alisema Mrimi.

 

Tembo wakivinjari  Serengeti 

Grumeti Fund yapunguza migogoro

ya binadamu, wanyamapori

 

Meneja Uhusiano, Mwakipesile, alisema taasisi ya Grumeti Fund kwa kushirikiana na serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) na idara za wanyamapori katika halmashauri za wilaya za Serengeti na Bunda zimekuwa vikifanya juhudi mbalimbali kupunguza migogoro kati ya binadamu na wanyampori.

 

“Kwanza tulifanya utafiti wa kubaini mapito na mwenendo wa tembo, kisha kwa kuhirikiana na TAWIRI tukawafungia tembo kifaa maalumu (collar) cha kufuatilia mwenendo wao,” alisema.

 

Ufutiliaji huo alisema umekuwa ukisadia kuzuia tembo kabla hawajavamia mazao ya chakula au kuingia kwenye makazi ya waanachi.

 

Lakini pia Grumeti Fund kwa kushirikiana na idara ya wanyamapori ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Kikosi Kazi didhi ya Ujangili Bunda (KDU) zimeanzisha kikosi maalumu cha kuzuia wanyamapori, hususan ambao wamekuwa wakivamia na kuharibu mazao ya wananchi.

 

“Lakini pia tumeanzisha free number (namba ya simu ya kupiga bure) ambayo wananchi hupiga simu saa 24 kutoa taarifa ya uwepo wa tembo katika maeneo yao na kupata msaada wa kuwafukuza kwa haraka,” alisema Mwakipesile.

 

Aidha, aliongeza kuwa wameendelea kutoa elimu kuhusu wanyamapori waharibifu katika vijiji vya wilaya za Serengeti na Bunda. ”Tunatoa elimu kupitia cinema, michezo, vikao na jarida letu la Sauti ya Grumeti,” alifafanua.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages