NEWS

Sunday 22 November 2020

Zifahamu hifadhi zilizobwagwa na Serengeti kwa ubora Afrika

Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

HIFADHI ya Taifa ya Serengeti (SENAPA) imeshinda Tuzo ya Hifadhi Bora zaidi barani Afrika kwa mwaka 2020 - ikizibwaga hifadhi tano za mataifa tofauti zilizoshiriki katika shindano hilo.

 

Tuzo hiyo ilitangazwa na Taasisi ya World Travel Awards (WTA) ya nchini Marekani kwa njia ya mtandao, Novemba 9, mwaka huu.

Kundi la tembo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

 

Hifadhi zilizoshindwa na SENAPA katika shindano hilo na nchi husika zikiwa kwenye mabano ni Central Kalahari (Botswana), Etosha (Namibia), Kidepo Valley (Uganda), Kruger (Afrika Kusini) na Maasai Mara (Kenya).

 

Hii ni mara ya pili kwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kushinda Tuzo ya Hifadhi Bora zaidi barani Afrika baada ya kutwaa ushindi huo katika shindano la aina hiyo mwaka 2019.

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa TANAPA, Pascal Shelutete, akizungumza katika moja ya mikutano ya wafanyakazi wa shirika hilo.

 

Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Pascal Shelutete, amesema SENAPA inajivunia fahari ya misafara ya nyumbu zaidi ya milioni 1.5 wanaohama na aina nyingine nyingi za wanyamapori wanaopatikana kwa wingi hifadhini.

 

Lakini pia, mandhari nzuri ya kuvutia na shughuli za utalii zinazovutia wageni wengi kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Simba wakipumzika na kufurahia upepo mwanana juu ya mti katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

“Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) linaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wananchi, wadau wa utalii na watu wote waliopiga kura zilizoiwezesha SENAPA kushinda Tuzo ya Hifadhi Bora zaidi barani Afrika kwa mwaka 2020,” amesema Shelutete.

 

Kwa upande mwingine, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo asilimia 70 ya eneo lake lipo mkoani Mara, ilishaingizwa kwenye orodha ya maajabu saba ya urithi wa dunia.

 

(Imeandikwa na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages