Simba wakiwa wamejipumzisha juu ya mti ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. |
HIFADHI ya Taifa ya Serengeti kupitia idara yake ya ujirani mwema, imetekeleza miradi 20 yenye thamani ya Sh bilioni 4.581 kwenye vijiji 26 ndani ya wilaya sita zinazopakana nayo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita (2009 – 2019).
Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richad akisisitiza jambo katika kikao na viongozi (hawapo pichani) wa kijiji cha Park Nyigoti wilayani Serengeti, hivi karibuni. |
Idara ya ujirani mwema ni mpango wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) unaolenga kuwafikia wananchi waishio jirani na Hifadhi kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya hadi mkoa ili kuwajengea uelewa na kuwafanya kuwa sehemu ya juhudi zinazofanywa na Shirika hilo katika uhifadhi wa maliasili na mazingira.
Lengo kuu la mpango huo ni kujenga uelewa wa jamii kuhusu umuhimu na faida zinazotokana na uhifadhi na kuiwezesha kunufaika na shughuli za uhifadhi ili kuifanya iwe sehemu ya jitihada zinazofanywa na TANAPA katika kulinda na kuhifadhi maliasili na mazingira ndani na nje ya Hifadhi.
Kwa mujibu wa Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard, miradi 20 iliyotekelezwa katika kipindi hicho ni ambayo iliibuliwa na wananchi wenyewe kupitia vikao mbalimbali katika vijiji husika - ikiwemo ya elimu, afya, barabara, maji na kiuchumi iliyo rafiki kwa mazingira.
“Wilaya zilizonufaika na mpango huo ni Serengeti, Tarime, Bunda (mkoani Mara), Ngorongoro (Arusha), Bariadi na Busega (Simiyu),” amesema Hobokela katika mahojiano maalumu na Sauti ya Mara ofisini kwake, hivi karibuni.
Viongozi na wakazi wa kata ya Kyambahi wilayani Serengeti katika picha ya pamoja na wahifadhi walipozuru katika kijiji cha Bokore kinachotarajiwa kutekelezewa mradi wa zahanati. |
Uwezeshaji shughuli za kiuchumi
Kuhusu mpango wa kuwezesha shughuli za kuinua kipatato cha wanavijiji, Mhifadhi Ujirani Mwema huyo anasema:
“Kwa kutambua changamoto ya hali ya umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi, Shirika [TANAPA] limejikita pia katika kuwezesha shughuli za kuinua kipato kwa wananchi kupitia kwenye vikundi.
“Pia kujenga uwezo wa wananchi kutengeneza mtaji ili kupata fursa za kupata mikopo midogo yenye riba nafuu na hii inafanyika kupitia mfumo wa Benki za Vijiji (COCOBA).”
Mpango huo, kwa mujibu wa Hobokela, umevigusa vikundi 117 vyenye wanachama 3,075 na hisa zenye thamani ya Sh bilioni 2.098 katika wilaya za Ngorongoro, Bariadi, Bunda, Serengeti na Meatu ya mkoani Simiyu.
Vikundi hivyo pia vimewezeshwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali iliyo rafiki kwa mazingira kama vile ufugaji nyuki, ambapo kwa mwaka wa fedha 2018/19 vikundi vinne vilivyopo Loliondo wilayani Ngorongoro vimepewa mizinga 120 na vifaa vyake na vinane vilivyopo Bariadi vimepewa mizinga 160 na vifaa vyake.
Matumizi bora ya ardhi
Hobokela anasema TANAPA kupitia idara ya Ujirani Mwema ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imewezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Matumizi Ardhi (NLUPC), ambapo vijiji 49 vilivyopo katika wilaya za Bariadi, Bunda na Tarime vimefikiwa.
Faida za mpango huo ni pamoja na kuongeza thamani ya ardhi ambapo inaweza kutumika kama dhamana kwenye mikopo, uwekezaji katika vijiji, kupunguza kama si kumaliza migogoro ya mipaka kati ya kijiji na kijiji, Hifadhi na vijiji, mtu binafsi na jirani yake, lakini pia kutatua kero ya wanyamapori waharibifu.
Kuhusu ajira kwa vijana kutoka vijiji jirani, anasema Hifadhi inaendelea kuongeza fursa hizo kwenye hifadhi, hoteli na kambi za kitalii, Maeneo ya Usimamizi wa Wanyamapori (WMA) na fursa ya soko la bidhaa zinazozalishwa na wananchi.
Watalii wakifurahia kutazama na kupiga picha makundi ya nyumbu katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. |
Hifadhi ya Taifa ya Serengeti yenye ukubwa wa kilomita za mraba 14,763 (sehemu kubwa ikiwa mkoani Mara), ilianzishwa mwaka 1959 kwa madhumuni ya kuhifadhi maliasili, kudumisha historia ya maisha ya binadamu na kuwa sehemu ya burudani.
Tembo wakifurahia mandhari ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti. |
Hifadhi hii inatambulika kama eneo la urithi wa dunia na ustiri wa maisha. Ni miongoni mwa Maajabu Mapya Saba ya Dunia. Imepata Tuzo ya Hifadhi Bora zaidi Barani Afrika kwa miaka miwili mfululizo (2019 na 2020) iliyotangazwa na World Travel Awards.
(Habari na picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment