NEWS

Tuesday 22 December 2020

TFS yawanoa wafugaji kuongeza uzalishaji, ubora mazao ya nyuki

Baadhi ya wafugaji nyuki wakifuatilia mafunzo ya mbinu za kuongeza uzalishaji na ubora wa mazao ya nyuki kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime.

 

WAFUGAJI 100 kutoka vikundi 50 vya ufugaji nyuki katika wilaya za Tarime, Musoma, Bunda, Serengeti na Butiama mkoani Mara, wamejengewa uwezo wa kuongeza uzalishaji, ubora na thamani ya mazao ya nyuki ikiwemo asali.

 

Aidha, wamehamasishwa kuanzisha chama cha ushirika kitakachowasaidia kutengeneza mtandao wa kupata masoko ya uhakika ndani na nje ya Tanzania.

Sehemu nyingine ya washiriki wa mafunzo hayo.


Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Ziwa na kufanyika katika ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime, Desemba 21, 2020.

 

Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoratibiwa na ofisi ya TFS Wilaya ya Tarime, Mhifadhi Misitu wa Wilaya hiyo, Charles Agustini Massawe amesema yatawasaidia wafugaji hao kufuga kisasa na kutengeneza mnyororo wa thamani ya mazao ya nyuki.

 

“Tumeona umuhimu wa kuendesha mafunzo haya kwa sababu ufugaji wa nyuki unasaidia kuhifadhi mazingira, kutunza misitu na kuepusha ukataji miti ovyo, lakini pia kumwondolea mfugaji umaskini wa kipato,” amesema Massawe.

Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Abel Mwita akihamasisha wafugaji nyuki kuanzisha chama chao cha ushirika.

 

Kwa upande wake, Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Abel Mwita amewahimiza wafugaji hao kuanzisha chama cha ushirika akisisitiza kuwa mbali na kuwawezesha kuunda mtandao wa kupata masoko, kitawaunganisha na vyama vingine vya kiuchumi.

 

Akisisitiza suala la soko la pamoja, Mwita amefafanua kuwa wateja wengi wanata asali nyingi iliyo bora na kutoka kwa chama cha ushirika kuliko kwa kikundi, au mfugaji mmoja mmoja.

Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mussa Robert akieleza faida za chama cha ushirika cha wafugaji nyuki katika mahojiano na Mara Online News.

 

Naye Afisa Ushirika wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Mussa Robert ametaja faida nyingine ya chama cha ushirika kuwa ni usimamizi wa pamoja wa ubora wa asali na mazao mengine ya nyuki kama vile nta.

 

Hata hivyo, akifunga mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri amewataka wafugaji hao kuhakikisha wanafuga kwa tija ili kujikwamua kiuchumi.

 

“Kikubwa hakikisheni mnafuga kwa tija na ongezeni bidii ya kupanda miti, ukikata mti, panda miti. Anzisheni chama cha ushirika kitawasaidia pia katika mpango wa kusindika asali,” amesema Mhandisi Msafiri.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri akihamasisha wafugaji wa nyuki kufuga kwa tija. Aliyekaa katikati ni Mhifadhi Misitu wa Wilaya ya Tarime, Charles Agustini Massawe.

 

Akizungumza na Mara Online News mara baada ya mafunzo hayo, kiongozi wa kikundi cha ufugaji nyuki cha Ikoma Cultural Centre, Agnes Makang’a ameshukuru kupata mafunzo hayo akisema yamemwelimisha mbinu za ufugaji wenye tija.

 

“Tumefundishwa kuchakata asali na kuyaongezea thamani mazao ya nyuki, pia tumefundishwa namna ya kuandaa na kutengeneza vifungashio bora vya asali, ninawashukuru TFS kutupatia elimu hii muhimu,” amesema Makang’a na kubainisha kuwa hadi sasa kikundi chao chenye wanachama 28 (wanawake 19 na wanaume tisa), kinamiliki mizinga 98 ya nyuki.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages