NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mwita Waitara amewaagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Apoo Castro Tindwa na Afisa Mazingira wa Halmashauri hiyo, Martha Mahule, kutumia Sikukuu ya Mwaka Mpya 2021 kufanya usafi kwa kuondoa takataka zinazohatarisha afya za wananchi katika soko la mji mdogo wa Sirari.
Waitara ametoa agizo hilo leo Desemba 31, 2020 alipokwenda kukagua mazingira na kushangazwa na marundo ya uchafu wa kila aina uliotapakaa jirani na vibanda vya kuuza matunda na migahawa katika soko hilo.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji, Tindwa, hakuwepo katika msafara wa Naibu Waziri Waitara wakati anatoa agizo hilo, aliyekuwepo ni Afisa Mazingira, Mahule.
Sehemu ya takataka zilizotapakaa jirani na vibanda vya biashara ikiwemo migahawa ya chakula katika soko la mji mdogo wa Sirari. |
Dampo hilo limekuwa kero kubwa kwa wafanyabiashara wa soko hilo kutokana na adha ya harufu kali ya uvundo unaohatarisha usalama wa afya za wafanyabiashara hao na wateja wao.
Nguruwe wakipata malisho katikati ya dampo la takataka katika soko la mji mdogo wa Sirari. |
Hali hiyo ya uchafuzi wa mazingira wa kutisha unaochangiwa na choo kilichotapakaa kinyesi cha binadamu hadi milangoni, ilimlazimu Naibu Waziri huyo kutoa tamko la kuhamisha jalala hilo haraka iwezekanavyo.
“Ninaagiza kwamba kesho [Januari 1, 2021] Afisa Mazingira na Mkurugenzi tuamkie hapa, uchafu uishe, choo kiwe safi, hiki kinyesi asubuhi nisikikute, na hili dampo marufuku hapa, lihamishiwe sehemu nyingine na liwekewe fence (uzio),” ameagiza.
Naibu Waziri Waitara amesema hawezi kuvumilia uchafuzi wa mazingira kama huo unaweza kusababisha magonjwa kwa wananchi ambao serikali ina jukumu la kuhakikisha wanakuwa na afya njema ili waweze kulipa kodi serikalini kutokana na shughuli zao mbalimbali.
Kwa upande mwingine, Waitara amepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wa soko hilo wanaotilia shaka ujenzi wa kibanda cha kuhifadhi takataka wakidai hauakisi thamani ya Sh milioni 60 zinazodaiwa kutumika.
Akijibu malalamiko hayo yaliyoungwa mkono na Diwani wa Kata Sirari, Amos Sagara, Naibu Waziri Waitara amewaahidi kulifuatilia akisema “Tutangalia nani amefanya kazi na nani hakufanya kazi yake, lazima tuwajibishane.”
Katika ziara yake ya kukagua mazingira leo, Naibu Waziri huyo anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira, pia aliagiza kufungwa kwa dampo la uchafu katika mtaa wa Starehe kutokana na kuwa katikati ya makazi ya wananchi.
Pia, Waitara ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kuondoa takataka zote zilizotupwa kandokando ya barabara mjini humo.
(Habari na picha zote na Mara Online News)
No comments:
Post a Comment