Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka (kushoto) akiteta jambo na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri James katika kikao kazi cha kujadili uelekeo wa mkoa huo. |
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amewataka viongozi wa kisiasa na serikali kushirikiana katika kuhakikisha ujenzi wa madarasa unakamilika kabla ya Januari ili kuwezesha wanafunzi waliofaulu wanapata vyumba za kusomea
Ameyasema hayo Desemba 12, 2020 wakati wa kikao kazi cha kujadili uelekeo wa mkoa wa Simiyu katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2020 - 20225) kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo afya, elimu, kilimo, viwanda na ajira kwa vijana - ambacho kimewashirikisha viongozi wa chama na serikali, wakuu wa idara, wafanyabiashara, viongozi wa dini, taasisi za umma na binafsi kilichofanyika kwenye ukumbi wa Bariadi Conference Centre mjini Bariadi, Simiyu.
Mbunge wa Itilima akichangia mada katika kikao hicho.
Mtaka ameongeza kuwa kwa maeneo ambayo yapo jirani na mapori ya akiba na migodi hakuna sababu za kuchangisha wananchi, badala yake fedha zinazotolewa zitumike katika ujenzi wa madarasa.
"Kakaeni kila mmoja na wadau wake, kuna maeneo hayana sifa ya kuchangisha michango ya madarasa, mfano Meatu kijiji cha Makao kuna mwekezaji wanachangia zaidi ya milioni 100 kwa mwaka - kuna haja gani ya kuchangisha wananchi," amesema na kuongeza kuwa:
"Kipaumbele cha hiyo pesa anzeni na madarasa, mfano maeneo ambayo ipo migodi ninachosema kila mmoja kwenye eneo lake mkae mjadili, madiwani ambao maeneo yenu migodi imeibuka zile asilimia zinazotolewa zielekezeni kwenye madarasa.”
Washiriki wa kikao hicho wakifuatilia mada.
Miriam Mmbaga ni Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, amesema japo mkoa huo umepanda kielimu kwa matokeo ya kitaifa - akitolea matokeo ya kidato cha nne ambapo mkoa umekuwa wa tatu kitaifa, bado kuna kazi ya kufanya ili wale wanaojifunza kwenye shule hizo waweze kujiajiri katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, walime kitaalamu ili tija ionekane na hatimaye wainue uchumi wao, wa mkoa na taifa kwa ujumla.
Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga akifafanua jambo kwenye kikao hicho.
Awali, akitoa ya elimu mkoani hapo kwa niaba ya Afisa Elimu Mkoa wa Simiyu, Jusline Bandiko amesema mkoa huo una mahitaji ya vumba vya madarasa 565, vilivyopo ni 419, huku upungufu ukiwa vyumba 155 ambavyo vinatakiwa kwa ajili ya kidato cha kwanza 2021.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Umoja wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Taifa, Kheri James ambaye pia ni Mlezi wa Mikoa ya Simiyu na Mara, amewataka viongozi mkoani hapo na kuendelea kudumisha umoja na mshikamano sambamba na kila mtu kufanya kazi na kutimiza wajibu wake - lengo likiwa kuwasaidia wananchi waliwaowapa dhamana ya uongozi.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Bariadi)
No comments:
Post a Comment