NEWS

Monday 28 December 2020

Muhongo asitisha mashindano ya ngoma kupisha ujenzi madarasa Musoma Vijijini

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo.

MBUNGE wa Musoma Vijijini mkoani Mara, Profesa Sospeter Muhongo, amesitisha mashindano ya ngoma za asili ambayo hufanyika kila mwisho wa mwaka ili kupisha ukamilishaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa jimboni humo.

 

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa jimbo la Musoma Vijijini linakabiliwa na upungufu wa yumba 31 vya madarasa kwa ajili ya wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2021.

 

Msaidizi wa Mbunge Muhongo jimboni, Fedson Magoma, ameiambia Mara Online News leo Desemba 28, 2020 kwamba hatua ya kusitisha mashindano ya ngoma za asili inalenga kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa linalowataka viongozi kuhakikisha wanafunzi wote waliochaguliwa kuanza masomo mwaka huu hawakosi vyumba vya madarasa.

 

Magoma amesema ofisi ya Mbunge Musoma Vijijini kwa sasa imejikita katika kuhamasisha wadau mbalimbali kushirikiana na wazazi kukamilisha ujenzi huo.

 

Amefafanua kwamba suala la elimu ni muhimu zaidi, hivyo Mbunge Muhongo ameamua kujikita huko kipindi hiki cha ukamilishaji wa vyumba vya madarasa.

 

Kwa mujibu wa msaidizi huyo wa mbunge, mashindano hayo ya kukuza utamaduni yatafanyika baada ya ujenzi wa vyumba hivyo kukamilishwa.

 

(Imeandikwa na Shomari Binda, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages