Baadhi ya wakazi wa kata ya Kyambahi na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika picha ya pamoja baada ya kikao chao kijijini Bokore, hivi karibuni. |
DIWANI wa Kata ya Kyambahi wilayani Serengeti, Herman Kinyariri amesema ujirani mwema na uhusiano wa vitendo kati ya wakazi wa kata hiyo na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni muhimu kwa uhifadhi endelevu.
Kinyariri ameyasema hayo katika kikao maalumu cha wakazi wa kijiji cha Bohore na watumishi wa Hifadhi hiyo hivi karibuni na kuweka wazi kuwa ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika kutekeleza miradi ya kijamii na kiuchumi utasaidia kupunguza kama si kutokomeza vitendo vya ujangili hifadhini.
Diwani wa Kata ya Kyambahi, Herman Kinyariri (kulia) akichangia mada katika kikao cha wakazi wa kijiji cha Bokore na watumishi wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti (hawapo pichani).
Wanakijiji wametumia nafasi hiyo pia kuikumbusha Hifadhi ya Serengeti kutekeleza ahadi ya ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho kwani tayari wameshasoma mchana na mawe.
Aidha, wananchi hao wameomba kusaidiwa katika kudhibiti tembo kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanaovamia kijiji cha Bokore na kuharibu mazao ya chakula mashambani.
Tembo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Wameomba pia kushirikishwa katika fursa za ajira hifadhini na kujengewa daraja litakalounganisha kijiji cha Bokore na kijiji jirani cha Park Nyigoti.
Akijibu hoja ya zahanati, Zabron Mtweve kutoka idara ya ujirani mwema katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, amewambia “Ahadi ya zahanati iko palepale, tumechelewa kutokana na mlipuko wa janga la Corona uliotokea, lakini ahadi hiyo iko palepale.”
Mtumishi wa idara ya ujirani mwema katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Zabron Mtweve.
Naye Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi hiyo, Hobokela Richard, amesema wanaendelea kukaribisha wawekezaji wa uhifadhi na utalii ili kupanua wigo wa kuchangia maendeleo ya wakazi wa vijiji jirani kikiwemo Bokore.
Mhifadhi Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Hobokela Richard akiwaeleza wakazi wa kijiji cha Bokore katani Kyambahi mipango ya kuimarisha ujirani mwema.
(Imeandikwa na Mara Online News, Serengeti)
No comments:
Post a Comment