NEWS

Wednesday 16 December 2020

TARURA Simiyu yazidai Meatu, Bariadi Vijijini mil 134/-

Mratibu wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Dkt Philemon Msomba akiwasilisha taarifa yake katika kikao hicho.


SERIKALI koani Simiyu imeombwa kusaidia Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (TARURA) mkoani humo ili halmashauri za Meatu na Bariadi Vijijini ziilipe Sh milioni 134. 

 

Mratibu wa TARURA Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Dkt Philimoni Msomba ameomba hilo Desemba 15, 2020 katika kikao cha Bodi ya Barabara.

 

“Tunawaomba viongozi wa mkoa mtusaidie kupata fedha hizo ili tuwalipe wanaotudai kwani halmashauri hizi zilitumia fedha hizi kutoka Mfuko wa Barabara maana baada ya TARURA kuanzishwa tulikuta tayari wamezitumia, tukaendelea kuwadai lakini mpaka leo bado hawajazirejesha.

 

“TARURA tunaidai Halmashauri ya Wilaya ya Meatu shilingi zaidi ya milioni 97.5, Bariadi Vijijini tunadai zaidi ya shilingi milioni 37.1, madeni haya ni tangu  mwaka 2017,” amefafanua Mhandisi Msomba.

 

Amesema kwamba katika mwaka wa fedha 2020/21, TARURA imepanga kutumia Sh bilioni 5.1 kugharimia ukarabati wa madaraja na barabara zenye urefu wa kilomita 822 na kuongeza kuwa Mfuko wa Barabara kwa sasa unapokea asilimia 30 huku Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wakipokea asilimia 70 ya bajeti ya matengenezo mbalimbali.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Simiyu akiwasilisha taarifa yake.

 

Katika hatua nyingine, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Simiyu, Mhandisi Albert Kent, akiwasilisha makisio ya bajeti ya mwaka 2020/21, amesema wanatarajia kutumia Sh bilioni 11.4 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zenye urefu wa kilomita 900 sambamba na madaraja.

 

Aidha, Mhandisi Kent ametaja vikwazo wanavyokutana navyo kuwa ni pamoja na baadhi ya wananchi kupitisha mifugo na kusababisha uharibifu wa barabara, lakini pia uvamizi wa hifadhi ya barabara unaofanywa na wajasiriamali wanaoweka bidhaa zao kwenye maeneo ya watembea kwa miguu, hali ambayo inaweza kusababisha ajali.

Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi akichangia mada katika kikao hicho.

Mkuu wa Wilaya ya Busega, Tano Mwera akichangia mada katika kikao hicho.

Baadhi ya washiriki wakifuatilia mada katika kikao hicho.


 (Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages