NEWS

Wednesday 16 December 2020

Waziri Mkenda asisitiza tija kwenye kilimo

Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika kikao hicho.

 

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amesema lazima kuongeza tija kwenye kilimo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji viwandani.


Profesa Adolf Mkenda akiendelea kuzungumza katika kikao hicho.

Profesa Mkenda ameyasema hayo Desemba 15, 2020 katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) Mkoa wa Simiyu kilichohusisha viongozi wa chama na serikali, idara za umma, taasisi binafsi na dini, kilichofanyika mjini Bariadi.

 

Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga, amesema mkoa huo umetenga hekta 61 wilayani Busega kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na kubainisha changamoto kubwa inayowakabili wakulima kuwa ni mitaji ambayo ingewawezesha kupata tija kwenye kilimo.


Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini ambaye pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery kilichopo mkoani Simiyu, Boaz Ogolla, amesema bado benki zinaendelea kutoza riba kubwa na kwamba wanapohoji sababu ya tozo hiyo wanaambiwa bado hawajapokea waraka wa maelekezo kutoka serikalini.

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho.


Naye Mbunge waVviti Maalum Mkoa wa Simiyu, Ester Midimu (CCM), amesema ujenzi wa viwanda utaongeza tija kwenye uzalishaji wa pamba na kupata uhakika wa soko la zao hilo.


Aswege Kaminyoge ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, yeye amesema bado kuna changamoto ya kupata mbegu za pamba za kutosha licha ya kwamba wamehamasisha wakulima wameitikia kulima zao hilo.


Mbali na hilo, Kaminyoge amesema pia bado kuna uhaba wa maafisa ugani, akitolea mfano wa wilaya ya Maswa yenye vijiji 120 lakini kati ya hivyo, 52 ndivyo vyenye wataalamu hao.


Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi, ametaka uwepo wa mkakati madhubuti wa kujua mkulima ana eneo gani na anahitaji kiasi gani cha mbegu ili kusaidia kumaliza tatizo la upungufu wa mbegu za pamba.

Sehemu nyingine ya washiriki wa kikao hicho.


Katika hatua nyingine, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba, amesema kuna kila sababu ya kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu wa kilimo.


"Baadhi ya wakulima wanalima bila kujua aina ya udongo, aina gani ya dawa inafaa kwa wakati huo, namna gani wakulima watapata fedha za mtaji ili walime kwa tija kwani kilimo ni mtaji, lakini pia wataalamu wajielekeze katika kutafuta masoko ya mazao ya wakulima,” amesema Kachwamba.

 

(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages