NEWS

Monday 14 December 2020

Viongozi waunguruma uzinduzi Baraza la Madiwani Tarime Mji

Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki (kulia), Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote (wa tatu kushoto), Katibu Tawala Wilaya ya Tarime, John Marwa (wa tatu kulia), Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa (wa pili kushoto) na viongozi wengine wakiimba Wimbo wa Taifa mara baada ya madiwani kula viapo mjini Tarime, leo Desemba 14, 2020.

 

HATIMAYE uzinduzi wa Baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara umefanyika leo Desemba 14, 2020 na kutoa fursa kwa viongozi mbalimbali kuhimiza ushirikiano na uwajibikaji katika kuwaondolea wananchi vikwazo vya maendeleo.

 

Shughuli ya viapo vya madiwani imesimamiwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa kwa kushirikiana na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya, Vicencia Balyaruha.

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msa

 

Katika hotuba yake, Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Mhandisi Mtemi msafiri amewataka madiwani hao kushirikiana na watumishi wa Halmashauri hiyo katika kuboresha huduma mbalimbali za jamii.

 

Mhandisi Msafiri ameitaka Kamati ya Afya kuelekeza nguvu kubwa katika kutafuta ufumbuzi wa huduma duni za matibabu na bei ghali ya dawa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime.

 

Aidha, amewahimiza madiwani hao kwenda kuhamasisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuwezesha wanafunzi kusoma bila msangamano kuanzia mwakani.

 

Mkuu huyo wa Wilaya ametumia nafasi hiyo pia kutoa onyo kwa wazazi wanaoozesha wanafunzi wa kike kipindi cha likizo na kusingizia kwamba wamewapeleka shule binafsi.

 

“Mzazi yeyote atakayepeleka mtoto wake shule binafsi lazima ahakikishe anakwenda kuripoti kwanza shule aliyofaulu na kutoa taarifa rasmi ya kumhamisha, tofauti na hapo sheria itachukua mkondo wake,” amesisitiza DC Msafiri.

Wananchi wakifuatilia viapo vya madiwani wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kwenye ukumbi wa MCN mjini Tarime, leo Desemba 14, 2020.

 

Mbunge wa Tarime Mjini, Michael Kembaki amewataka madiwani wote kutambua kuwa wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanakidhi kiu ya maendeleo ya wananchi waliowaamini na kuwachagua.

 

“Inapaswa sisi tulioaminiwa na Chama pamoja na wananchi tuwatendee haki wananchi katika kata zote kwani wana matarajio makubwa ya kuletewa maendeleo,” amesema Kembaki.

 

Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mara, Ghatty Chomete, amesema “Huu ni muda wa kuwatumikia wananchi kama ambavyo walituamini wakatuchagua, hivyo tukawatumikie ili waone kile walichokitarajia kwetu, sio muda wa kushangilia tena, ni muda wa kuwajibika.”

Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote (katikati), Katibu Tawala Wilaya ya Tarime, John Marwa (kulia) na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa (kushoto) wakiwa makini kwa ajili ya kuanza kuimba Wimbo wa Taifa wakati wa uzinduzi wa Baraza jipya la Madiwani wa Halmashauri hiyo kwenye ukumbi wa MCN mjini Tarime, leo Desemba 14, 2020.

 

Kwa upande wake, Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote, amneaahidi madiwani ushirikiano wa dhati na kuwahimiza kushirikiana na wananchi katika kuwaletea maendeleo ya kisekta.


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marema Soro, yeye ametumia nafasi hiyo kuwahimiza madiwani hao kutanguliza maslahi ya wananchi mbele na kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Chama hicho tawala katika maeneo yao ya uongozi.                                     

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye (Namba tatu) akizungumza katika kikao hicho cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime.

 
                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                     
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samweli Kiboye maarufiu kwa jina la Namba Tatu, amewataka madiwani hao kujenga uhusiano na watumishi wa Halmashauri hiyo kwa umakini na kuepuka mgawanyiko usio na maslahi ya umma.

 

“Nendeni mkashirikiane na watumishi na sio kuwatukana na kuwadhalilisha, kashirikianeni kuchapa kazi kama Rais wetu Dkt John Pombe Magufuli anavyochapa kazi katika kuleta maendeleo ya wananchi, kwa pamoja inawezekana,” amesisitiza Namba Tatu.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages