Profesa Adolf Mkenda akizungumza katika kikao hicho. |
WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda, amesema lazima kuongeza
tija kwenye kilimo kwa ajili ya kuongeza uzalishaji viwandani.
Profesa Adolf Mkenda akiendelea kuzungumza katika kikao hicho. |
Profesa Mkenda ameyasema hayo Desemba 15, 2020 katika Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) Mkoa wa Simiyu kilichohusisha viongozi wa chama na serikali, idara za umma, taasisi binafsi na dini, kilichofanyika mjini Bariadi.
Awali, Katibu Tawala Mkoa wa Simiyu, Mariam Mmbaga, amesema
mkoa huo umetenga hekta 61 wilayani Busega kwa ajili ya kilimo cha
umwagiliaji na kubainisha changamoto kubwa inayowakabili wakulima kuwa ni
mitaji ambayo ingewawezesha kupata tija kwenye kilimo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba nchini ambaye
pia ni Meneja wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Ginnery kilichopo
mkoani Simiyu, Boaz Ogolla, amesema bado benki zinaendelea kutoza riba kubwa na
kwamba wanapohoji sababu ya tozo hiyo wanaambiwa bado hawajapokea waraka wa
maelekezo kutoka serikalini.
Sehemu ya washiriki wa kikao hicho. |
Naye Mbunge waVviti Maalum Mkoa wa Simiyu, Ester Midimu (CCM), amesema ujenzi wa viwanda utaongeza tija kwenye uzalishaji wa pamba na kupata uhakika wa soko la zao hilo.
Aswege Kaminyoge ni Mkuu wa Wilaya ya Maswa, yeye amesema bado kuna changamoto
ya kupata mbegu za pamba za kutosha licha ya kwamba wamehamasisha wakulima
wameitikia kulima zao hilo.
Mbali na hilo, Kaminyoge amesema pia bado kuna uhaba wa maafisa ugani, akitolea
mfano wa wilaya ya Maswa yenye vijiji 120 lakini kati ya hivyo, 52 ndivyo
vyenye wataalamu hao.
Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi, ametaka uwepo wa mkakati madhubuti
wa kujua mkulima ana eneo gani na anahitaji kiasi gani cha mbegu ili kusaidia
kumaliza tatizo la upungufu wa mbegu za pamba.
Sehemu nyingine ya washiriki wa kikao hicho. |
Katika hatua nyingine, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Simiyu, Haula Kachwamba, amesema kuna kila sababu ya kuendelea kutoa elimu kwa wakulima ikiwa ni pamoja na kuongeza wataalamu wa kilimo.
"Baadhi ya wakulima wanalima bila kujua aina ya udongo, aina gani ya
dawa inafaa kwa wakati huo, namna gani wakulima watapata fedha za mtaji ili
walime kwa tija kwani kilimo ni mtaji, lakini pia wataalamu wajielekeze katika
kutafuta masoko ya mazao ya wakulima,” amesema Kachwamba.
(Imeandikwa na Anita Balingilaki, Simiyu)
No comments:
Post a Comment