NEWS

Friday 15 January 2021

Gimmy amimina misaada ya kielimu Serengeti, DC Babu aipokea kwa shangwe

 

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu (wa pili kushoto) akipokea msaada wa madawati na viti vyake kwa ajili ya wanafunzi kutoka kwa Diwani wa Geitasamo, Joshua Nyansiri aliyemwakilisha mdau wa maendeleo, Gimmy James Mgaya aliyetoa msaada huo.

KAMPUNI ya Gimmy Inter Co. Ltd yenye makao makuu jijini Dodoma, leo Januari 15, 2021 imetoa misaada mbalimbali yenye thamani ya Sh milioni 14.85 kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya elimu wilayani Serengeti, Mara.

Diwani wa Geitasamo, Joshua Nyansiri (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu msaada wa saruji mifuko 100 iliyotolewa na Gimmy James Mgaya kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule wilayani humo.

Misaada hiyo ni pamoja na madawati 30 na viti vyake - vyote vyenye thamani ya Sh milioni 2.4, saruji mifuko 100 (Sh milioni 2.2), fedha taslimu Sh milioni 1.25 za kununua mabati 50 na eneo la ukubwa wa ekari tatu lenye thamani ya Sh milioni tisa kwa ajili ya upanuzi wa Shule ya Msingi Nyamerama.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu (wa pili kushoto mbele) akiwa amepokea msaada wa Sh milioni 1.25 kutoka kwa Diwani wa Geitasamo, Joshua Nyansiri (kulia) - uliotolewa na mdau wa maendeleo, Gimmy James Mgaya kwa ajili ya kununua mabati 50 ya kuezeka majengo ya shule wilayani humo.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Gimmy Co. Ltd, Gimmy James Mgaya amewakilishwa na Diwani wa Kata ya Geitasamo, Joshua Nyansiri ambaye amekabidhi misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu.

 

Akizungumza katika hafla ya makabidhiano hayo, Diwani Nyansiri amesema Gimmy ametoa misaada hiyo kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli katika kuboresha sekta ya elimu nchini.

Madawati 30 na viti vyake - vilivyotolewa msaada na mdau wa maendeleo, Gimmy James Mgaya kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa shule za sekondari wilayani Serengeti.
 

Mkuu wa Wilaya, Babu, amemshukuru Mkurugenzi huyo wa Gimmy Co. Ltd kutokana na misaada hiyo na kutumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wadau wengine kuiga mfano huo kwa kujitokeza kuchangia maendeleo ya elimu wilayani Serengeti.

 

Naye Afisa Elimu Sekondari Wilaya ya Serengeti, Mwalimu Simon Mdaki amewataka wakuu wa shule zilizolengwa na misaada hiyo kuhakikisha inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti (wa kwanza kushota aliyekaa) na Diwani wa Geitasamo, Joshua Nyansiri (aliyekaa katikati) na viongozi wengine wakifurahia madawati na viti vyake - vilivyotolewa msaada na mdau wa maendeleo, Gimmy James Mgaya kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa shule za sekondari wilayani humo.

Baada ya hapo, Babu amekabidhi misaada hiyo kwa maofisa watendaji wa kata za Geitasamo, Machochwe, Mosongo, Nyambureti na Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kuigawa kwenye shule husika.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages