NEWS

Sunday 31 January 2021

Mara wajipanga kufuta ukatili, unyanyasaji wa kijinsia

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Vicent Naano (aliyesimama) akifungua kikao cha RCC mjini Musoma, leo Januari 31, 2021. Aliyekaa kulia ni Katibu Tawala Mkoa wa Mara, Catherine Mtapula.

SERIKALI mkoani Mara inafikiria kuwa na mpango mkakati maalumu wa kudhibiti na kupambana na matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

 

Matukio hayo ni pamoja na ukeketaji yanayoendekezwa miongoni mwa jamii katika baadhi ya wilaya za mkoa huo.

 

Changamoto hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Vicent Naano wakati akifungua Kikao cha Ushauri cha Mkoa (RCC) kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima mjini Musoma, leo Januari 31, 2021.

 

Dkt Naano amesema matukio ya ukatili na unyanyasaji yanauchafua mkoa huo, hivyo kuna haja ya kujipanga kuwa na mkakati maalumu wa wa kuyakabili na kuyakomesha.

 

“Ndugu zangu ukatili wa kijinsia na ukeketaji bado ni tatizo kwenye mkoa wetu, hivyo ni muhimu kuja na mkakati wa kudhibiti matukio haya. Tujadiliane kwa kina na baadaye kupata ushauri na namna ya kufanya ili kuondoa hili linalotia doa mkoa wetu wa Mara,” amesema Dkt Naano.

 

Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa wilaya ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kwa kuongoza Tanzania nzima katika utoaji asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.

 

Kiongozi huyo ametoa wito kwa halmashauri nyingine kuongeza nguvu ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kutoa mikopo kwa makundi hayo ya jamii kama ilivyokwisha kuelekezwa na serikali.

 

(Imeandikwa na Shomari Binda, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages