NEWS

Sunday, 15 February 2026

Tarime: Giza nene mnada wa mifugo Magena



Sehemu ya miundombinu ya mnada wa mifugo Magena ambao haujafunguliwa kwa miaka kadhaa sasa

Na Mwandishi Wetu,
Tarime
-------------

Licha ya serikali kutumia mamilioni ya shilingi kuboresha mnada wa mifugo Magena uliopo katika Halmashauri ya Mji wa Tarime mkoani Mara, mnada huo haujawahi kufunguliwa kwa miaka kadhaa sasa.

Viongozi na wananchi wa eneo hilo wanaiomba serikali kufungua mnada huo ili uweze kuwakwamua kichumi.

“Huu mnada ungekuwa umefuguliwa, uchumi wa watu wetu ungekuwa mzuri, tunashangaa umetumia mamilioni ya fedha na bado miuondombinu yake inalindwa na kampuni ya ulinzi lakini hautumiki tangu mwaka 2022,” mmoja wa wananchi na mfanyabiashara wa Mageni aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara juzi.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Magena ni miongoni mwa minada 10 ya mpakani inayosimamiwa na wizara hiyo nchini.

Mnada huo upo takriban kilomita 10 kutoka mpaka wa Sirari unaotenganisha Tanzania na Kenya.

Naibu Waziri wa Mifugo, Ng’wasi Damas Kamani, alikiambia kikao cha Bunge jijiji Dodoma Januari 29, 2026 kuwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 serikali ilitumia shilingi milioni 175.65 kugharimia ujenzi wa miundombinu mbalimbali ya mnada huo - kama vile mazizi, kipakilio, birika la maji na vyoo.

Naibu Waziri huyo alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko, aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuendeleza mnada huo.

Lakini viongozi na wananchi wa eneo hilo wanasema mnada huo haujawahi kufunguliwa tangu ulivyoboreshewa miundombinu wakidai umetelekezwa.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages