NEWS

Wednesday 13 January 2021

Wananchi 42 wakabidhiwa hati miliki za viwanja Musoma

Mwananchi (kushoto) akipokea hati miliki ya kiwanja kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Vcent Naano, jana Januari 12, 2021.

WANANCHI 42 katika Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara wameishukuru Serikali kwa kuwakabidhi hati miliki za viwanja vyao.

 

Hati hizo ni kati ya 142 zilizoandaliwa na idara ya ardhi katika Manispaa hiyo kipindi hiki baada ya kufunguliwa kwa ofisi ya ardhi ya mkoa.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Januari 12, 2021 mara baada ya kukabidhiwa hati hizo na Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Dkt Vicent Naano, wananchi hao wamesema wamefarijika kuzipata.

 

Wamesema mwanzoni upatikanaji wa hati miliki za viwanja ulikuwa na mzunguko mrefu lakini kwa sasa wametumia muda mfupi kuzipata.

 

Mmoja wa wananchi hao, Damian Manyonyi, amesema kufunguliwa kwa ofisi ya ardhi ya mkoa inayosimamiwa na Kamishna Msaidizi wa Ardhi kumekuwa msaada wa kuwezesha wananchi kupata hati hizo kwa urahisi.

 

Akikabidhi hati hizo kwa wananchi, Mkuu wa Wilaya, Dkt Naano, amesema naye amefarijika kuona sasa zinapatikana kwa urahisi wilayani hapa.

 

Naano amesema kabla ya kufunguliwa kwa ofisi ya ardhi ya mkoa, wananchi walikuwa wakitumia gharama kubwa kusafiri kwenda ofisi za kanda mkoani Simiyu kufuatilia hati miliki.

 

“Serikali imeamua kuwasaidia wananchi wake kwa kupata hati miliki kwa muda muafaka na zinawafanya kuaminika, na mnaweza kukopesheka, kikubwa ni kuzitunza vizuri,” amesema.

 

Kwa upande wake, Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Mara, Jerome Kiwia, amesema ni muhimu kuzingatia kulipa kodi za viwanja na kuwaomba waliopewa hati miliki kuwajulishga wengine kuwa siku hizi zinapatikana kwa muda mfupi.

 

(Imeandikwa na Shomari Binda, Musoma)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages