NEWS

Friday 26 February 2021

Mbunge Ghati: Bajeti Tarime Mji imegusa kila mwananchi

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete akizungumza na Mara Online News mjini Tarime, leo Februari 26, 2021.

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete, ameeleza kuridhishwa na bajeti ya Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa mwaka wa fedha 2021/2022 akisema imegusa kila mwananchi wa halmashauri hiyo inayoongozwa na Mkurugenzi Elias Ntiruhungwa.

 

Akizungumza na Mara Online News mjini Tarime leo Februari 26, 2021 baada ya baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kupitisha bajeti ya Sh bilioni 30.222, Ghati amesema bajeti hiyo imelenga kuboresha miradi ya kijamii na kiuchumi kwa manufaa ya halmashauri na wananchi wake.

 

“Bajeti hii imegusa pia soko, tunaenda kupata soko zuri sana la kisasa, soko litakalozungukwa na vibanda vitakavyokodishwa kwa wafanyabiashara na kuiwezesha halmashauri kupata mapato,” amesema mbunge huyo.

 

Uchangiaji ujenzi wa soko la kimkakati la mji wa Tarime ni miongoni mwa vipaumbele vya mpango na bajeti ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

 

Vipaumbele vingine ni pamoja na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya halmashauri kwa njia ya kielektroniki, kuboresha huduma za elimu na afya, na kutekeleza mkakati wa lishe bora unaohusisha kutenga Sh 1,000 kwa ajili ya kila mtoto mwenye umri chini ya miaka mitano.

Kutoka kulia ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, John Marwa, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Elias Ntiruhungwa, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote na Makamu wake, Thobias Ghati wakishiriki kikao cha baraza la madiwani.
Baadhi ya madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime wakishiriki kikao hicho.

Kwa upande mwingine, Mbunge Ghati ameahidi ushirikiano wa dhati kwa wananchi na serikali katika kubuni na kutekeleza miradi ya kisekta ili kustawisha uchumi wa mkoa wa Mara na Taifa kwa jumla.

 

Ametumia nafasi hiyo pia kuwambia wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime na mkoa wa Mara kuratajia miradi zaidi ya kimaendeleo itakayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.

 

“Mimi naiamini serikali yetu, hasa Rais wetu Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli - akisema anatekeleza. Kwa hiyo mimi ninawaaminisha wananchi wa wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kutegemea mambo makubwa mazuri kutoka Serikali hii ya Awamu ya Tano, Serikali ya viwango na vitendo,” amesisitiza Mbunge Ghati.

 

(Habari na picha: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages