NEWS

Thursday 25 February 2021

World Vision yakabidhi zahanati Ikungulipu

Kaimu Meneja wa World Vision Kanda ya Nzega, Klasta Gilselda Balyafati akikabidhi vifaa tiba na dawa kwa Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi, kwa ajili ya zahanati ya Ikungulipu.

WAKAZI wa kijiji cha Ikungulipu katika wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, wameondokana na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya baada ya Shirika la World Vision Tanzania kuwakabidhi zahanati.


Ujenzi wa zahanati hiyo umegharimu Sh milioni 110.565 ambazo ni michango ya nguvu kazi na baadhi ya vifaa kutoka kwa wananchi, huku World Vision wakichangia gharama za ujenzi (kumlipa mkandarasi ) na ufuatiliaji  uliofanywa na wahandisi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima. 


Hayo yamesemwa jana Februari 24, 2021 na Kaimu Meneja wa Kanda ya Nzega, Klasta Gilselda Balyagati wakati wa makabidhiano ya jengo la zahanati hiyo na miundombinu yake na kuongeza kuwa wamekabidhi vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Sh milioni 5.1 kwenye zahanati ya Ikungulipu.

 

Pia zahanati ya Senani iliyo ndani ya mradi imekabidhiwa vifaa tiba na dawa vyenye thamani ya Sh milioni 1,909 kwa ajili ya kuboresha huduma za afya kwenye zahanati hizo. 

 

"Ujenzi ulianza mwaka 2015 ambapo World Vision Tanzania kupitia Luguru Area Program (Luguru AP) kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Ikungulipu mradi ulikamilika, wananchi walichangia mawe, mchanga, maji na kokoto na ilianza kufanya kazi Machi 2020," amesema Balyagati.


Awali, akisoma taarifa ya hali ya huduma za afya kwenye zahanati ya kijiji cha Ikungulipu, Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Dkt Yohana Nzize amesema wana changamoto ya watoa huduma ambapo mpaka sasa wapo wawili, huku ikama ya watumishi ikitaka kila zahanati kuwa na watoa huduma 15, jambo ambalo ni kikwazo, hasa pale mmoja wao anapopata dharura au likizo.


Mbali na changamoto hiyo, zahanati hiyo inahudumia wakazi 14,634 wa vijiji vya Ikungulipu na Giriku.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Luguru, Jongela amesema wakazi wa kijiji cha Ikungulipu wamekuwa wakipata adhara ya kutembea umbali wa kilomita 15 kufuata huduma kwenye zahanati ya Luguru.

 

"Kijiji hiki ni kikubwa, kina vitongoji 10, awali wananchi walitembea umbali mrefu kufuata huduma, baadhi ya kina mama walijifungulia njiani, mvua ilipokuwa ikinyesha idadi kubwa ya wananchi walishindwa kufika kwenye huduma, lakini sasa mambo hayo yamekwisha baada ya kukamilika kwa zahanati hii," amesema Jongela.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza kushuhudia makabidhiano ya zahanati.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Dkt Anold Musiba amesema wilaya hiyo ina zahanati 30 za serikali, vituo vya afya vitatu na hospitali ya wilaya ambapo wananchi wanapata huduma zilizo bora zaidi.

 

Mratibu wa World Vision Luguru, Betty Isaack amesema Luguru Area Program (Luguru AP) ni mradi wa maendeleo ya jamii ambao unafanya kazi kwenye eneo husika ambalo ni kata za Luguru na Nhobora.


Amefafanua kuwa mradi huo ni wa miaka 15 ambapo na kwa sasa una miaka tisa na unalenga kuwafikia watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi, familia na jamii kwa ujumla huku akisisitiza kwamba walengwa namba moja ni watoto, hasa wanaoshi katika mazingira hatarishi.


Akijibu changamoto zilizotajwa kwenye taarifa iliyosomwa na Mganga Mfawidhi wa zahanati hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Itilima, Benson Kilangi amewahakikishia wananchi wa kijiji hicho upatikanaji wa huduma ya umeme, maji na nyumba ya mganga mfawidhi.

 

 (Habari na picha zote na Anita Balingilaki, Itilima)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages