NEWS

Thursday 11 February 2021

Ni neema tupu Tarime Vijijini. Mgodi walipa bilioni 2, DC Msafiri ahimiza ziboreshe huduma za jamii

Kutoka kulia ni Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Luiz Correia, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion K Samwel, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Apoo Castro Tindwa, Meneja Mahusiano wa Mgodi huo, Gilbert Mworia na Katibu Tawala wa Wilaya hiyo, John Marwa.

MGODI wa Barrick North Mara, leo Februari 11, 2021 umelipa ushuru wa huduma (service levy) kiasi cha Sh 2,090,183,849 kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

 

Kampuni ya uchimbaji madini ya Twiga Minerals iliyoundwa kwa ushirikiano wa kampuni ya madini ya Barrick na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia mgodi huo - imekabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha kwa Halmashauri hiyo - ikiwa ni ushuru wa huduma kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2020.

Makabidhiano ya hundi hiyo yakiendelea.

Akikabidhi hundi hiyo, Meneja Mkuu wa Mgodi wa Barrick North Mara, Luiz Correia amesema “Tunapokabidhi fedha hizi leo tunaona fahari kwa kuwa tumeendelea kushuhudia matunda ya matumizi sahihi ya fedha katika kuboresha miundombinu inayochangia kuimarisha uchumi na huduma muhimu kwa watu.”

 

Correia ameongeza “Kipimo cha mafanikio kupitia mchango wa mgodi wa dhahabu wa North Mara ni kuona matokeo endelevu yanayolenga kuimarisha huduma za jamii na maendeleo ya kiuchumi kwa jamii nzima.”

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Luiz Correia (wa pili kushoto) akizungumza baada ya makabidhiano hayo.

Sambamba na ushuru huo, mgodi huo umechangia kupeleka maendeleo katika vijiji 11 vinavyouzunguka, ambapo mchango huo umejikita katika kuimarisha huduma za elimu, afya, maji, miundombinu na miradi ya kiuchumi iliyoibuliwa na jamii husika.

 

“Tunampongeza sana Mkuu wa Wilaya [Msafiri] kwa kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji, pia tunawapongeza viongozi wetu wengine wa Serikali na wananchi kuanzia ngazi za vijiji, kata, halmashauri na mkoa wetu wa Mara kwa ushirikiano na juhudi tunazoziona za kusimamia vizuri matumizi ya fedha za ushuru wa huduma tunazolipa kila baada ya miezi sita.

Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Luiz Correia (wa pili kushoto) akiendelea kuzungumza baada ya makabidhiano hayo. Wa kwanza kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri.

“Juhudi hizo zinatuhamasisha kufanya kazi zaidi ili kuzalisha zaidi na tulipe ushuru mkubwa, hivyo kuendelea kuchangia zaidi maendeleo chanya katika wilaya yetu ya Tarime (Vijijini) na mkoa wa Mara kwa ujumla.

 

“Kampuni yetu kwa kushirikiana na Serikali na wadau wengine wa maendeleo ndani na hata nje ya nchi, itaendelea kujenga jamii endelevu ili kuendana na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano na Dira ya Taifa kufikia mwaka 2025,” ameongeza Meneja huyo wa Mgodi wa North Mara.

 

Akipokea hundi hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri amesema “Tuna imani kwamba fedha hizi zitatumika kuboresha huduma za jamii, hasa elimu, afya na maji,” amesema Msafiri na kuongeza:

 

“Tarime sasa inakimbia kimaendeleo, tunataka kila shule ya sekondari ya kata iwe na hosteli, ufaulu katika mitihani ya taifa unaendelea kuongezeka, nia na lengo ni kuhakikisha hakuna division zero (alama sifuri).”

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhandisi Mtemi Msafiri (wa pili kulia) akizungumza baada ya makabidhiano hayo.
 

Hadi sasa wilaya ya Tarime ina shule za sekondari 57 zikiwamo sita za kidato cha sita - kati ya hizo, nne ni za wasichana na mbili za wavulana. Shule za sekondari za wasichana ni Borega, Ingwe, Manga na JK Nyerere, na shule za sekondari za wavulana ni Tarime na Magoto.

 

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Apoo Castro Tindwa amesema ofisi yake itaendelea kutumia mapato ya ndani zikiwemo fedha za ushuru wa huduma zinazotolewa na mgodi huo kuboresha huduma za jamii.

 

Tindwa ameweka wazi kuwa uboreshaji wa huduma za afya ni miongoni mwa vipaumbele vya Halmashauri hiyo yenye vituo vya afya vinane.

Ilivutia sana wakati wa makabidhiano hayo.

Migodi ya dhahabu inayoendeshwa na kampuni ya Barrick hulipa ushuru wa huduma kila baada ya miezi sita kwa halmashauri ambazo migodi hiyo inaendesha shughuli zake, kulingana na mapato ya kila mwaka.

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages