NEWS

Tuesday 2 February 2021

Wabunge watumie kwa uwazi fedha za Mfuko wa Jimbo

Deo Meck

MFUKO wa Jimbo ulianzishwa kisheria na kupitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2009 kwa lengo la kuchochea maendeleo ya jimbo.

 

Maendeleo yanayolengwa hapa ni miradi mbalimbali ya kijamii na kiuchumi inayoanzishwa na wananchi katika majimbo yao.

 

Fedha za Mfuko huo zinatolewa na Serikali Kuu kama mchochezi mkuu wa maendeleo nchini.

 

Fedha hizo hudhibitiwa na kamati maalum ya watu saba, na Mbunge ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo. Fedha hizo haitakiwi zitumike bila kuidhinishwa na kamati hiyo ya watu saba chini ya uenyekiti wa Mbunge.

 

Mbunge na kamati yake ndio wenye kauli na maamuzi ya mwisho juu ya matumizi ya fedha za Mfuko huo.

 

Hata hivyo, katika baadhi ya majimbo nchini, Mfuko huo umekuwa ukitumika kisiasa kuliko malengo yaliyokusudiwa wakati unanzishwa.

 

Wabunge wengi wamekuwa wakitumia fedha za Mfuko huo wakiwadanganya wananchi kuwa hizo ni fedha zao binafsi.

 

Matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo yanahitaji uwazi na ushirikishaji wananchi ili malengo ya kuanzishwa kwake yatimie.

 

Kama nilivyoainisha hapo juu lengo la kuanzishwa kwa Mfuko huo ni kuchochea maendeleo katika majimbo ya uchaguzi, si vinginevyo. Hapo chini nitaeleza ni jinsi gani Mfuko huo umekuwa ukitumika ndivyo sivyo ili kumsaidia au kumjenga Mbunge kisiasa.

 

Kimsingi matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo inapaswa yaende sambamba na kuwiana na vipaumbele vya halmshauri ya mji, wilaya au manispaa.

 

Lakini kinyume na malengo ya uanzishwaji wake, wabunge wengi wamekuwa wakiutumia Mfuko huo kwa manufaa yao binafsi kisiasa kwa njia kuu mbili.

 

Kuna wakati Mbunge anachangia shughuli za maendeleo; mathalani kupeleka saruji katika ujenzi wa shule. Lakini badala ya Mbunge kusema fedha hizo zimetoka kwenye Mfuko wa Jimbo anasema ni zake binafsi.

 

Njia ya pili; tunaelewa katika jamii kuna vikundi na vyama mbalimbali vya kijamii ambavyo malengo yake yanaishia katika mipaka ya wanachama wa vikundi hivyo.

 

Kuna wabunge wasio waaminifu ambao huchukua fedha za Mfuko wa Jimbo na kwenda kuchangia katika vikundi hivyo huku wakijinasibu kuwa ni fedha zao binafsi.

 

Mambo hayo yamefanyika hata mkoani Mara, hususan katika majimbo ya Tarime Mjini na Rorya kwa muda mrefu - tangu mwaka 2015 hadi sasa.

 

Lakini pia kuna wabunge ambao wamechukua fedha za Mfuko wa Jimbo na kuchangia ujenzi wa nyumba mbalimbali za ibada huku wakiwadanganya waumini kuwa ni fedha zao binafsi - ili kujionesha ni wakarimu.

 

Kwa hiyo ushirikishwaji wa wananchi katika matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo ambazo kimsingi ni kodi zetu umekuwa haufahamiki.

 

Kumekuwa na siri na kificho kikubwa sana kwenye mgawanyo wa fedha za Mfuko huo ambazo zingeweza kuchochea maendeleo kwa kutumika katika miradi ya kimkakati inayogusa jamii nzima.

 

Ni kinyume cha sheria na ni kinyume cha malengo ya uanzishwaji wa Mfuko wa Jimbo - kwa Mbunge kuutumia kwa malengo yake binafsi ya kisiasa na kwa shughuli nje ya kuchochea miradi ya maendeleo inayogusa jamii nzima.

 

Miradi mingi ya wananchi inakwama kwa sababu ya kukosa kichocheo muhimu kama hicho ambacho Serikali iliona umuhimu wake na ikaamua kukileta.

 

Nitoe wito kwa Serikali kuanza kuweka utaratibu mzuri wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo kwani ni dhahiri kuwa nyingi hazitumiki kwa malengo yaliyokusudiwa.

 

Hata jimbo la Tarime Mjini ninakotokea mwaka huu fedha za Mfuko wa Jimbo zimeendelea kutumika lakini hakuna uwazi wa kuonesha zimetoka wapi.

 

Fedha hizo zinatumika kama vichaka vya wabunge kutoshiriki shughuli za maendeleo na baadaye hudanganya wananchi kuwa zimetoka mifuko yao binafsi.

 

Ni jukumu letu sisi wananchi kuwabana wabunge na wateule katika hiyo kamati kujua kiasi cha fedha ambacho kimekuja katika majimbo yetu na kutaka kujua matumizi yake.

 

Na ingelikuwa jambo la busara zaidi kwa Mbunge na kamati yake kuweka utaratibu wa kuwashirikisha wananchi katika matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo.

 

Kukiwa na uwazi katika rasilimali zinazokuja katika majimbo na wilaya zetu ni rahisi kujua tumepata nini na kiende wapi.

 

Kwa uzoefu wa zaidi ya miaka kumi toka Mfuko huo uanzishwe unatosha kuona mapungufu yaliyopo na kuyafanyia kazi.

 

Na ikiwezekana ni bora katika hiyo kamati kuu ya watu saba, kukawa na halmashauri ya kamati hiyo ambayo itawahusisha madiwani wa kata zote maana wao ndio wawakilishi wa kata zao na wanajua changamoto za kimaendeleo zinazokabili kata zao.

 

Au la, basi ni heri mapendekezo ya matumizi ya fedha za Mfuko wa Jimbo baada ya mapendekezo ya hiyo kamati ya Mbunge na watu wake, yapelekwe kwenye baraza la madiwani kwa ajili ya kupitishwa.

 

Ushirikishwaji wa kiwango hicho utaleta uwazi na ushirikishwaji mpana kuliko kuwaachia watu wachache ambao kimsingi hadi sasa wameonesha udhaifu katika kusimamia fedha za Mfuko huo.

 

Kwa sababu kama zinatumika ndivyo sivyo na wajumbe wengine wa kamati wako kimya ina maana kuna namna na wao pia wananufaika na fedha za Mfuko huo, hivyo wanachagua kukaa kimya ili waendelee kufaidika kwa gharama za wananchi kukosa maendeleo.

 

Kuna miradi mingi ya maendeleo ambayo Mfuko wa Jimbo ukitumika vyema tutaweza kufanikisha mengi, hususan miradi ya elimu, afya, maji na mingine mingi ya kuweza kuwavusha wananchi.

 

Hivyo ni jukumu letu sote kama wananchi kuhakikisha kuwa tunashiriki katika ulinzi wa rasilimali zetu zikiwamo fedha za Mfuko wa Kuchochea Maendeleo ya Jimbo.

 

Uchambuzi huu umechapishwa kwa mara ya kwanza kwenye Gazeti la Sauti ya Mara - toleo la Jumatatu Februari 1, 2021.

 

(Umeandikwa na Deo Meck 0715481628)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages