NEWS

Monday 22 February 2021

Waitara aendeleza kasi ya kutekeleza ahadi Tarime Vijijini

Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (kulia) akikabidhi msaada wa saruji mifuko 10 kwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kiterere, Jacob Adongo (kushoto) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya zahanati ya kijiji hicho, jana.

MBUNGE wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameendeleza kasi ya kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ambapo jana Februari 22, 2021 ameanza mpango wake wa kugawa misaada ya saruji na mabati kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya miradi mbalimbali ikiwemo ya elimu na afya jimboni humo.

 

Akizungumza wakati wa makabidhiano ya baadhi ya vifaa hivyo vya ujenzi, Waitara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), amesema amejipanga kugawa saruji mifuko 660 na mabati 600.

Mbunge Waitara (kulia) akikabidhi msaada wa saruji mifuko 15 kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Bumera, Joseph Ryoba (kushoto) kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Sekondari ya Kurumwa.
 

Miradi iliyoanza kupata mgawo wa saruji jana ni Shule ya Sekondari ya Regicheri ambayo Mbunge Waitara ameipatia mifuko 40, Shule ya Msingi Keroti (mifuko 40) na Shule ya Sekondari ya Nyarotambe (mifuko 20).

 

Amegawa pia saruji mifuko 15 katika Shule ya Sekondari ya Kurumwa na kwenye mradi wa zahanati ya kijiji cha Kiterere amegwa saruji mifuko 10.

Mbunge Waitara (mwenye koti ya suti katikati) akikabidhi msaada wa saruji mifuko 40 kwa Diwani wa Kata ya Susuni, Wambura Matiko (kushoto) kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Shule ya Msingi Keroti.

Waitara ametumia nafasi hiyo pia kuwashukuru wadau waliomuunga mkono katika upatikanaji wa vifaa hivyo vya ujenzi huku akisisitiza kuwa kipaumbele chake ni kusikiliza kero za wapigakura wake (wananchi wa Tarime Vijijini) na kuzitafutia ufumbuzi.

 

Januari 2021, Mbunge Waitara alifanya ziara ya kukagua maemndeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule za sekondari mbalimbali jimboni na kuchangia gharama za ujenzi huo.


Baadhi ya shule za sekondari alizotembelea na kiasi cha fedha alichochangia kikiwa kwenye mabano ni Bukenye (milioni 10), Kewamamba (milioni saba) na Regicheri (milioni tano).

 

(Habari na picha zote na Mara Online News)

 

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages