NEWS

Sunday 14 March 2021

ATFGM Masanga, viongozi wa dini waungana kukataa ukatili wa kijinsia

Viongozi wa madhehebu na mashirika ya dini katika semina ya kujadili na kuweka mikakati ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani Tarime.
 

SHIRIKA lisilo la Serikali la ATFGM Masanga limewakutanisha viongozi wa madhehebu na mashirika ya dini wilayani Tarime, Mara kuainisha vyanzo vya ukatili wa kijinsia na hatua za kuchukua kuutokomeza katika jamii.

 

Warsha hiyo imefanyika mjini Tarime Machi 12, 2021 ikiwa ni mwendelezo wa juhudi za Shirika la ATFGM Masanga za kuhamasisha jamii kuunganisha nguvu ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia vikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni.

Majadiliano yakiendelea.
 

Washiriki wa warsha hiyo wametaja vyanzo vya vitendo vya ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na umaskini, mila potofu, tabia ya kurithi na ukosefu wa elimu ya Mungu.

 

Mchungaji Peter Mahe wa EAGT Itiryo, amefafanua kuwa umaskini umesababisha baadhi ya watu wakiwemo ngariba (wakeketaji) na wazee wa mila kuendelea kukumbatia mila ya ukeketaji kama mradi wa kujipatia kipato cha kujikimu na familia zao.

 

Kuhusu elimu ya Mungu, Mchungaji Samwel Chacha wa Kanisa la PEFA Nyamombela amesema watu wasio na elimu hiyo hawana hofu ya Mungu, hali inayowasababisha kutenda mambo ya kishetani ukiwemo unyanyasaji wa kijinsia.

Mshirikia akichangia mada.
 

Mchungaji wa Samwel Mohabe wa Kanisa Anglikana Tarime yeye amesema tabia ya kurithi inachangia kwa kiasi kikubwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

 

“Mfano, mtoto anakuwa anajua baba kumpiga mama ni jambo la kawaida, au kukeketa mtoto wa kike ni lazima. Mtoto anakua anajua kwamba kazi hii ni ya mwanamke pekee - hata kama inamkandamiza,” amesisitiza Mchungaji Mohabe.

 

Naye Askofu Paul Baru wa Kanisa la Jesus Great Hope Nyamisangura B, amesema hata kasumba ya kuwatenga, kuwalaani na kutowaoa watoto wa kike waliokeketwa inachangia kuendelea kwa vitendo hivyo katika jamii.

 

Kwa upande mwingine, wanasiasa wamelaumiwa katika warsha hiyo kwamba wengi wao wamekuwa wakilipa nguvu suala la ukeketaji kwa lengo la kujipatia maslahi yao binafsi ikiwemo kupigiwa kura za ndiyo wakati wa kugombea uongozi.

 

“Lakini pia pia ni wazi kwamba hata Serikali yetu imelegeza nguvu ya kusimamia marufuku ya ukeketaji,” amesema mmoja viongozi hao wa kiroho.

 

Hata hivyo, Emmanuel Omenda kutoka Shirika la ATFGM Masanga amesema waathirika wengi wa vitendo vya ukatili wa kijinsia wamekuwa wakikosa ujasiri wa kwenda kulalamika kwenye vyombo vya sheria kutokana na mfumo dume uliojengeka katika baadhi ya familia kama si jamii.

Kiongozi wa kiroho (kulia) akichangia mada.

Washiriki hao wamesema inawezekana kupunguza kama si kutokomeza mila na desturi hizo zenye madhara katika jamii ikiwa Serikali, viongozi wa kiroho na amashirika ya dini, wanasiasa na jamii kwa ujumla watashirikiana kuvikataa kwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wanaovikumbatia.

 

Wameongeza kuwa ushirikiano wa makundi hayo uhusishe pia utoaji elimu ya Mungu na kuhamasisha wanaume kuacha kuoa mabinti waliokeketwa.

 

Washiriki hao wamehitimisha warsha hiyo kwa kuweka mpango mkakati wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia utakaohusisha kukemea mfumo dume, kutumia vipindi vya dini kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na kuelimisha ngariba na wazee wa mila adhabu zinazoweza kuwakumba kutokana na makosa ya kuendekeza ukeketaji na ndoa za utotoni.

Sehemu nyingine ya washiriki wa warsha hiyo.
 

Warsha hiyo imewashirikisha pia Mkurugenzi wa ATFGM Masanga, Sista Bibiana Bokamba na Meneja Miradi wa shirika hilo, Valerian Mgani.

 

Warsha hiyo imekuja siku chacha baada ya shirika hilo kuandaa na kuendesha nyingine ya kujadili ukeketaji na madhara yake - iliyowashirikisha viongozi wa idara mbalimbali katika maeneo ya mpakani upande wa Tanzania na Kenya.

 

Hii ni baada ya kubainika kwamba kumekuwepo na watu ambao baada ya kufanya ukatili wa kijinsia ama wamekuwa wakimbilia kujificha Kenya, au Tanzania ili kukwepa mkono wa sheria.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages