NEWS

Tuesday 23 March 2021

Dkt Wanyancha amlilia Dkt Magufuli, asema alikaribia kuifikisha Tanzania kwenye orodha ya nchi zilizoendelea

Dkt James Wanyancha

ALIYEKUWA Naibu Waziri katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, Dkt James Wanyancha, ameelezea kuumizwa na kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt John Pombe Magufuli akisema kiongozi huyo alikuwa amebakiza muda mfupi kuifikisha Tanzania kwenye hadhi ya nchi iliyoendelea.

 

“Kama angetupigia miaka mitano mingine, angeiacha nchi yetu pazuri sana. Hii nchi chini ya uongozi wake ilikuwa imebakiza sehemu fupi kufikia hatua ya nchi iliyoendelea,” amesema Dkt Wanyancha katika mahojiano na Mara Online News kwa njia ya simu, juzi.

 

Dkt Wanyancha aliyepata kuwa Mbunge wa Serengeti mkoani Mara na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi enzi ya uongozi wa Rais Kikwete, amesema Dkt Magufuli alikuwa miongoni mwa watu wachache wenye maono na uwezo mkubwa wa kutenda mambo ya kiaendeleo.

 

“Nimefanya naye kwa karibu sana kwa miaka mitatu akiwa Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na mimi nikiwa Naibu wake, baadaye nikiwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara nchini kwa miaka sita, hivyo ninamfahamu vizuri, alikuwa na vision kubwa sana, uwezo wake ulikuwa mkubwa mno na akishaamua anatekeleza,

 

“Huyu bwana alikuwa na vision (maono) ambayo alikuwa anaweza kufikiria kitu na kikitenda kweli, Alikuwa mtu shupavu wa kusimamia mambo ya maendeleo. Ni watu wachache wenye vision kubwa na huwezi kumfahamu mpaka atekeleze.

 

“Nimeumia sana kutokana na kifo cha Rais wetu Dkt John Magufuli, Mambo mengi yalikuwa yameshindikana lakini yeye ameyatekeleza ikiwemo kuhamishia makao makuu jijini Dodoma na kukamilisha ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere kule Kwangwa, nje kidogo ya mji wa Musoma,” amesema Dkt Wanyancha.

 

Dkt John Pombe Magufuli wakati wa uhai wake

Dkt Wanyancha amesema daima atambukuka Rais Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ukiwemo wa uzalishaji umeme katika mto Rufiji, uanzishaji wa ujenzi wa reli ya kisasa na ununuzi wa ndege kadhaa kwa kutumia fedha za ndani.

 

Pia utekelezaji wa miradi ya kimakakati ikiwemo ile ya ujezi wa meli mpya, ukarabati wa MV Victoria na MV Butiama na uanzishaji wa ujenzi wa daraja la Kigogo Busisi katika Ziwa Victoria, lakini pia kuendeleza udhibiti wa vitendo vya ufisadi dhidi ya mali za umma.

 

“Ninampa pole mjane wa Dkt Magufuli, mama Janet, familia yake na mama yake mzazi kwa sababu ni watu ambao wananifahamu sana,” amesema Dkt Wanyancha.

 

Dkt Wanyancha ametumia nafasi hiyo pia kumtakia kila la kheri Rais Samia Suluhu Hassan akisema ana imani kwamba atavaa viatu vya Rais Magufuli kwa kuendeleza msukumo wa kusimamia ukusanyaji mzuri wa kodi na kuielekeza kwenye miradi ya maendeleo ya wananchi.

 

(Habari: Mara Online News)

Habari hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Sauti ya Mara, Machi 22, 2021.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages