NEWS

Wednesday 3 March 2021

LHRC yawajengea wanahabari uwezo wa kusaidia kulinda haki, amani

Baadhi ya waandishi wa habari na maafisa wa LHRC katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa semina ya kuwajengea uwezo wa kusaidia kulinda haki na amani.

IMEELEZWA kwamba watu wengi wamekuwa wakiingia katika migogoro kutokana na kutotambuana.

 

Hayo yameelezwa na Afisa Vijana wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Ally Seif Ramadhani wakati akiwezesha semina ya siku tatu kuwajengea waandishi wa habari uwezo wa kusaidia kulinda na kutetea haki na amani katika jamii.

Mwezeshaji wa semina hiyo, Ally Seif Ramadhani (katikati) akiwa kazini.

Semina hiyo iliyoanza Machi 2, 2021 kwenye hoteli ya APC jijini Dar es Salaam, inaendeshwa na LHRC kwa kushirikiana na Shirika la Search for Common Ground kupitia mradi wa Jenga Amani Yetu, na inawashirikisha waandishi wa habari 25 kutoka mikoa ya Mara, Pwani na Mtwara.

 

“Watu wanaingia kwenye migogoro kwa kutotambuana, wakishatambuana wanaona hawana sababu ya kugombana, wengi huwa ni wamoja ila wanatofautiana kwa majina,” amesisitiza Ally Seif Ramadhani.

 

Mwezeshaji huyo amesema haki na amani ni zao la watu waliojenga dhana ya kusikilizana na kutambuana.

Sehemu ya washiriki wa semina hiyo.

Naye Mratibu Mradi wa Jenga Amani Yetu, Caroline Shoo amesema amani inadumishwa pale watu wote wanapojiona ni wamoja na kila mmoja kutambua ana wajimu wa kujenga na kulinda amani.

 

“Kila mmoja anapaswa kujiona ni sehemu ya kujenga amani. Ni vigumu kuepuka migogoro lakini tunaweza kuepuka vurugu katika jamii zetu,” amesema Shoo.

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Uwezeshaji na Uwajibikaji wa LHRC, Felista Mauya, Afisa Vijana wa kituo hicho, Ally Seif Ramadhani na Mratibu Mradi wa Jenga Amani Yetu, Caroline Shoo.

Awali, akifungua semina hiyo, Mkurugenzi Uwezeshaji na Uwajibikaji wa LHRC, Felista Mauya amesema itawasaidia waandishi wa habari na vyombo vya habari kuwa sehemu ya suluhisho la migogoro katika jamii.

Mkurugenzi Uwezeshaji na Uwajibikaji wa LHRC, Felista Mauya akifungua semina hiyo.
Mkurugenzi Uwezeshaji na Uwajibikaji wa LHRC, Felista Mauya (wa tano/katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wanawake walioshiriki semina hiyo.
 

Semina hiyo imeendeshwa chini ya ufadhili wa Jumuiya ya Ulaya (EU).

 

(Habari na picha zote na Christopher Gamaina, Dar es Salaam)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages