NEWS

Sunday 14 March 2021

Mamia ya wananchi wamiminika mlima Balili, wahamasishwa kutembelea Hifadhi ya Serengeti

Sehemu ya mamia ya wananchi wa wilayani Bunda waliojitokeza kupanda mlima Balili, jana.

WANANCHI zaidi ya 300 wengi wao wakiwa vijana na wanafunzi kutoka shule za msingi na sekondari, kikundi cha skauti, vyuo na taasisi mbalimbali katika wilaya ya Bunda mkoani Mara, wamejitokeza kupanda mlima Balili - ikiwa ni mojawapo ya juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani.

 

"Tukio hilo limeandaliwa na kampuni ya NCT - TWENDE KUTALII kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na Radio Mazingira FM 91.7," amesema Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Albert Chenza.

 

Limefanyika jana Machi 13, 2021 kati ya saa mbili asubuhi na saa 10 jioni - ambapo wananchi hao wamemudu kutembea umbali wa kilomita 16 kupanda na kushuka mlima huo kwa miguu - wakiongozwa na viongozi wa serikali wilayani Bunda na wale yenye dhamana ya utalii na uhifadhi kutoka hifadhi hiyo.

Safari ya kukwea mlima Balili ikiendelea.
 

Aidha, tukio hilo limehusisha upandaji miti, upigaji picha za kumbukumbu katika maeneo tofauti ya mlima huo na utoaji wa huduma za kupima afya ikiwemo ya kupima mapigo ya moyo bila malipo.

Mmoja wa wanafunzi waliotembelea mlima Balili akipanda mti jirani na majengo ya hoteli inayotoa huduma kwa wageni mlimani hapo.
 

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malime amekuwa akiutaja mlima Balili kama mlima wa kimakakati na kivutio kikubwa cha utalii wilayani Bunda kutokana na upekee wa mazingira yake yanayowezesha mtu awapo kileleni kuona kwa uzuri zaidi mawio (kuchomoza) na machweo (kuzama) ya jua, lakini pia kuangalia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Ziwa Victoria.

Kikundi cha Skauti kilianzisha safari ya kupanda mlima Balili kwa kuimba na kucheza nyimbo za kitaifa.
 

Akizungumza na Mara Online News mlimani hapo, mwanafunzi wa kidato cha tano kutoka Shule ya Sekondari ya Bunda, Abdallah Ramadhani amesema tukio hilo limempa burudani ya kipekee na kumwezesha kujifunza mambo mengi.

 

“Nilikuwa nasikia sifa za mlima Balili, leo nimeamua kufika ili nijionee mwenyewe. Nimeona miti ya aina mbalimbali yenye majina ya kibaiolojia. Mfano nimeona mti unaoitwa Mheche na mingineyo.

 

“Mazingira ya huu mlima ni mazuri, kuna miamba mikubwa inayovutia, nimefika kwenye kilele cha mlima huu na kuweza kuona Hifadhi ya Serengeti upande wa Mashariki na Ziwa Victoria upande wa Kaskazini Magharibi. Kwa ujumla mazingira hayo yanapendeza sana upande wa Serengeti na ziwa.

 

“Nikipata chance (nafasi) nyingine nitarudi, maana nime- enjoy (nimefurahi) sana. Nashauri vijana wenzangu tuwe wazalendo kwa vya kwetu na tuvitangaze wenyewe,” amesema mwanafunzi huyo.

Baadhi ya vijana waliojitokeza kukwea mlima Balili wakiangalia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wakiwa katika kilele cha mlima huo.
 

Mkazi wa mjini Bunda, Veronica Masunga naye ameelezea furaha yake ya kukwea mlima Balili hadi kileleni na kutumia nafasi hiyo kutoa wito kwa vijana wengine kupanga safari za kutembelea mlima huo.

 

“Nimefurahi kupanda mlima huu wa Balili hadi kileleni, ni mara yangu ya kwanza kufika huku, nimejifunza vitu vingi sana - nimeona jinsi mlima ulivyokaa kwa kuvutia na nimeona Hifadhi ya Serengeti. Kwa ujumla nimefurahi sana na ninatamani kurudi huku siku nyingine. Vijana wengine nao wasichelewe, waje kujionea kivutio hiki cha utalii,” amesema Veronika.

Baadhi ya watalii wa ndani kutoka mjini Bunda waliojitokeza kutembelea mlima Balili wakipunga hewa juu ya mlima huo.
 

Mwananchi mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Yusuf Kayumba ameeleza kuridhishwa na mambo mengi katika tukio hilo la kupanda mlima Balili. Ameshauri taasisi za elimu kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali wilayani Bunda na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti katika kuhamasisha utalii wa ndani mlimani na hifadhini.

 

“Nimejifunza vitu vingi, kwanza wananchi, hasa vijana wameonesha mwamko mkubwa wa kujitokeza kutembelea mlima huu, na hili pia ni suala la afya kwa maana ya kufanya mazoezi ya kutembea umbali wa kilomita zaidi ya 16 kupanda na kushuka kwa miguu.

 

“Mazingira yanavutia kuanzia chini hadi juu ya mlima huu wa Balili na kuna vitu vingi vya kuangalia. Nashauri shule za msingi, sekondari na vyuo vijiwekee mpango wa kudumu wa kuwaleta wanafunzi huku kutalii na kujifunza mambo mbalimbali, kuona miamba na mlima ulivyopangika kwa mvuto wa aina yake,” amesema Kayumba.

Wana-Bunda wengine wakipanda mlima Balili.

Akizungumza na wananchi hao waliofanya utalii wa ndani juu ya mlima Balili, Afisa Tarafa ya Kenkombyo, Rebecca Mdodo ambaye pia anakaimu nafasi hiyo katika tarafa ya Nansimo wilayani Bunda, amesema tukio hilo limepata mwitikio mkubwa zaidi ya ilivyotarajiwa.

 

“Wananchi wameonesha mwamko mkubwa wa kufanya utalii wa ndani. Ninaamini tukio hili litahamasisha wana-Bunda wengi kutembelea mlima huu wa Balili, lakini pia mlima Chamriho hapa Bunda,” amesema Mdodo.

Afisa Tarafa ya Kenkombyo, Rebecca Mdodo naye akifurahia mandari ya mlima Balili.

Afisa Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George amesema tukio hilo limekuwa fursa nzuri ya kuhamasisha wananchi wa Bunda kushiriki masuala ya utalii na uhifadhi.

 

“Tumepanda mlima Balili ambao ni kivutio kikubwa ndani ya wilaya ya Bunda. Sisi kama wadau wa utalii kutoka Hifadhi ya Taifa ya Serengeti tunaona hii ni fursa muhimu sana, na tunaona sasa wilaya imeanza kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano katika kukuza utalii katika nchi yetu.

 

“Kwa tukio hili, wilaya ya Bunda imeonesha mfano mzuri na kuweka historia kubwa kwa kuanza kushiriki kwa vitendo - kwa kuhakikisha vijana na wana-Bunda kwa ujumla wanauenzi utalii. Utalii ni hamasa na utalii ni burudani," amesema Mhifadhi Tutindaga.

Mhifadhi Tutindaga George akizungumza wananchi wa Bunda (hawapo pichani) waliotembelea mlima Balili. Anayeonekana nyuma ni Mkurugenzi wa kampuni ya NCT - TWENDE KUTALII, Albert Chenza.

Mhifadhi Tutindiga ameongeza “Sisi kama wadau wa utalii tunaona kwamba kundi kubwa la vijana au wana-Bunda takriban 300 waliojitokeza leo ni fursa ambayo sasa tunaweza kuitumia kulihamasisha liwe linapanga safari kila mwaka ikiwezekana kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

 

“Lakini kwa kuanzia, mwezi ujao [Aprili] tunayo Sikukuu ya Pasaka, kwa hivyo kama hifadhi tunashirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na ofisi ya DAS (Katibu Tawala wa Wilaya) kuandaa safari maalum kwa ajili ya wana-Bunda kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kipindi hiki package (tozo) yetu ni shilingi 40,000 kwa kila Mtanzania kutembelea hifadhi.

 

“Lakini kikubwa zaidi, hifadhi inaenda kuandaa bonanza maalumu kwa ajili ya wana-Bunda ambao watajitokeza kipindi hiki cha Pasaka kutembelea hifadhi. Hii ni kwa ajili ya kuleta umoja, tunasema utalii ni hamasa na burudani. Kwa hivyo tunaendelea kuhamasisha utalii wa ndani ili kuwapata wananchi wengi ambao wataunga mkono hawa waliojitokeza leo."

Sehemu ya vijana kutoka Bunda waliotembelea mlima Balili wakimshikiliza mhifadhi (hayupo pichani) juu ya mlima huo.
 

“Mlima Balili ni kivutio cha kipekee kama unavyoona mandhari ya hapa tulipo. Kwanza tunasema kupanda mlima ni suala la kiafya, utalii ni afya, utalii ni kuburudika. Ukipanda huu mlima unaona mazingira ambayo huwezi kuyaona mahali pengine. Lakini kikubwa zaidi ukifika mahali hapa unaona vizuri Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na kwa upande mwingine unaona Ziwa Victoria ambalo ni maarufu sana.

 

“Kwa hivyo, Watanzania wahamasike kutembelea vivutio vilivyopo wilaya ya Bunda, hasa huu mlima na watembelee pia Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo mengine yenye vivutio mkoani Mara. Utalii unaanza na sisi wenyewe,” amesema Mhifadhi Tutindaga George.

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande unaopakana na wilaya ya Bunda - inavyoonekana kutokea kwenye kilele cha mlima Balili.

Naye Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Neema Mollel amesema matunda ya kushirikiana na wadau yameanza kuonekana - akitolewa mfano wa wananchi hao wa Bunda waliojitokeza kutembelea mlima Balili.

 

“Tunaendelea kushirikiana na viongozi wa serikali ma wadau wengine katika wilaya ya Bunda katika kuhamasisha utalii wa ndani, ndio maana tumefanikiwa kuandaa kundi hili kubwa lililopanda mlima huu wa Balili. Ninawashukuru wadau tulioshirikiana nao vizuri katika kufanikisha hili.

 

“Kikubwa zaidi leo tumekuja kuangalia vivutio vilivyopo kwenye mlima huu, lakini pia kuhamasisha wananchi waweze kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambayo iko karibu sana na Bunda," amesema Kamishina huyo.

Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii, Neema Mollel akihutubia wananchi hao (hawapo pichani)  juu ya mlima Balili.
 

“Tunaamini kwa kushirikiana, utalii utaendelea na watu wengi katika mji huu wa Bunda watahamasiska kufanya utalii wa ndani," amesema Kamishna huyo na kuendela:

 

“Tunaendelea na program nyingine kwa ajili ya kuwezesha... Tunaomba wananchi wajitokeze kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, lakini pia waje kutembelea kivutio hiki cha mlima Balili na Ziwa Vichtoria. Unafuu tunaotoa kwa watalii wa ndani ni kwamba hawalipi gharama kubwa kama watalii wanaotoka nje ya nchi.

 

“Unajisikiaje kuona uko jirani na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti lakini haujaitembelea. Ninawaomba wananchi msiishie kuona wanyamapori mnapokuwa mnasafiri barabarani kwenye mabasi ya abiria, jitokezeni kufanya utalii wa ndani. Utalii ni kwa ajili yetu wote,” amesisitiza Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii, Neema Mollel.

Kutoka kulia ni Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Utalii wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Neema Mollel,
Mhifadhi Mkuu na Mkuu wa Kitengo cha Utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Tutindaga George na Afisa Habari wa TANAPA Kanda ya Magharibi, Brigitha Kimario wakifurahia mandari ya mlima Balili.
 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

1 comment:

  1. kazi nzuri mmefanya
    naweza nikapata namba kamishna wa hifadhi

    ReplyDelete

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages