NEWS

Monday 8 March 2021

Mbunge Ghati akazia elimu kwa mtoto wa kike, achangia madawati 50

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete akihutubia wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani wilayani Tarime, leo.

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Zephania Chomete ametumia maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika wilayani Tarime, kusisitiza jamii kukazania elimu kwa watoto wa kike.

 

Akihutubia katika maadhimisho hayo yaliyofanyika kiwilaya katani Nyamwaga leo Machi 8, 2021, Mbunge Ghati ambaye amekuwa mgeni rasmi, amesema mwanamke ni mtu muhimu na chachu ya maendeleo ya jamii, hivyo kuelimisha mtoto wa kike ni kuelimisha dunia nzima.

Mbunge Ghati (kulia mbele) akishirikiana na wanawake wengine kuimba na kucheza wakati wa maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani.

“Lazima tuhakikishe shule ya wasichana Nyamwaga inajengwa ili watoto wetu wapate elimu bora. Akina mama ni jeshi kubwa, ukimuinua mtoto wa kike, umeinua jamii nzima, kwa hiyo lazima wanawake tuungane na tuinuane,” amesema mbunge huyo kijana.

 

Katika kuunga mkono juhudi za kuwezesha elimu, Ghati ameahidi kutoa mchango wa madawati 50 kwa ajili ya shule za halmashauri ya wilaya ya Tarime.

Mbunge Ghati akiendelea kuhutubia.

Pia, Mbunge Ghati amehimiza umuhimu wa jamii kuwashirikisha wanawake kikamilifu katika nyanza zote za kimaendeleo.

 

Mbunge Ghati ametumia nafasi hiyo pia kuitaka jamii kuepuka vitendo vya unyanysani na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, lakini pia kuachana na mila zilizopitwa na wakati ukiwemo ukeketaji watoto wa kike.

 

Ghati alimpongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Apoo Castro Tindwa kwa kuwawezesha akina mama kupata mikopo mbalimbali na kuwasisitiza akina mama ambao wapo kwenye vikundi, kuchukua mikopo ili iweze kuinua uchumi wao.

Wanafunzi nao walihudhuria maadhimisho hayo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Apoo Castro Tindwa ameitaka jamii kumthamini mwanamke akisema kila penye mafanikio yoyote kuna mkono wa mwanamke.

Mkurugenzi Mtendaji Apoo akizungumza katika maadhimisho hayo.

Mwanasheria wa Shirika lisilo la Kiserikali linalotoa elimu juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia la ATFG Masanga, Dora Luhimbo amesema wamefanikiwa kuokoa wasichana wengi kwa kuwapeleka kwenye kambi okozi kwa ajili ya kuwapatia elimu na msaada wa kisheria.

 

Naye Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nyamwaga, Fatma Mbwana ameomba ushirikiano wa jamii nzima katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijimnsia dhidi ya watoto wa kike na wanawake.

Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Nyamwaga, Fatma Mbwana naye alipata nafasi ya kuzungumza katika maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani.

Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema “Wanawake katika Uongozi: Chachu ya Kufikia Dunia yenye Usawa.”

 

(Imeandikwa na Lilian Tesha wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages