NEWS

Monday 15 March 2021

Sekta ya umwagiliaji inavyoweza kututoa tukiiboresha

Miche ya kahawa kwenye kitalu

NI wazi kuwa asilimia zaidi ya 80 ya Watanzania wameendelea kujihusisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara, ingawa kundi kubwa ni wakulima wadogo wadogo na wachache ni wakulima wa kati na wakubwa.

 

Utegemezi wa mvua pekee,kwa ajili ya kilimo umekuwa ukisababisha uzalishaji mdogo wa mazao ya chakula na biashara katika maeneo mengi nchini.

 

Sisi kama Taifa tufikie mapinduzi ya kijani kwa ajili kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara. Hatuna budi kuhakikisha sekta ya umwagiliaji ambayo kwa sasa huitwa Tume ya Umwagiliaji ya Taifa inapewa msukumo mkubwa wa ujenzi wa miundombinu yake

 

Serikali iendelee kutenga bajeji ya kutosha kwa ajili ya kujenga miundombinu mikubwa na midogo ya umwagiliaji ambayo ni pamoja na mabwawa na malambo makubwa ya maji katika kila halmashauri nchini ili wakulima wengi wazalishe kwa tija na kuinua Taifa kiuchumi.

 

Hiyo itachangia kuwezesha nchi yetu kupanda kutoka hadhi ya uchumi wa kati kuingia uchumi wa juu.

 

Serikali Kuu na halmashauri zetu kama ziongeze kasi ya kujenga miundombinu ya maji na kuwezesha wakulima wengi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha kwa riba nafuu ili waweze kununua zana za kilimo kama vile trekita na majembe ya kukokotwa na wanyama.

 

Pia, mikopo hiyo itawezesha wakulima kumudu ununuzi wa pembejeo kama vile mbolea, mbegu na viuatilifu

 

Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Singida, Tabora, Manyara na Dodoma huitwa mikoa kame kutokana na kupata mvua chini ya mm 1,000 kwa mwaka katika baadhi ya halmashauri.

 

Mikoa hiyo ipewe kipaumbele katika ujenzi wa mabwawa na malambo ya maji kwa ajili ya kuendesha kilimo cha umwagiliaji.

Wakulima wakikagua shamba la pamba katika moja ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

 

Bado kuna maeneo yanayofaa kuwekeza katika kilimo cha mazao ya chakula na biashara kwa wingi, hivyo kuchangia kuipaisha Tanzania kuelekea uchumi wa juu.

 

Ninasisitiza mambo haya kwa sababu Serikali yetu ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli ni Serikali ya viwanda, na viwanda vinahitaji sana malighafi zinazotokana na kilimo.

 

Mikoa ya Mbeya, Katavi, Ruvuma, Iringa na Morogoro huitwa “The Big Five” kwa kilimo cha mazao ya chakula na biashara. Lakini kuna haja ya kuongeza mikoa mingine ya kuzalisha kwa wingi mazao hayo.

 

Mfano, mikoa ya Shinyanga na Simiyu inafaa sana kwa kilimo cha pamba, mpunga na alizeti, mtama, mahindi, dengu, karanga, choroko na njugu mawe.

 

Pamoja na hali hiyo kuna changamoto ya viwanda vikubwa vya kuchakata pamba na kukamua mafuta ya alizeti katika mikoa hiyo.

 

Asilimia 60 ya mbegu za pamba nchini huzalishwa katika mikoa ya Simiyu na Shinyanga, lakini mikoa hiyo haina kiwanda kikubwa cha nguo na nyuzi zitokanzo na zao hilo. Hii ni changamoto kubwa kwa wakulima katika maeneo hayo.

 

Wadau wa kilimo wanaishauri Seikali  Kuu na halmashauri nchini kulipa kipaumbele cha kwanza suala la kuwekaza kwenye sekta ya umwagiliaji/tume ya umwagiliaji kwa kujikita zaidi katika kujenga skimu zenye mifereji imara, kuongeza nguvu ya kifedha na utalaamu, huku nguvu kubwa ikielekezwa kwenye mikoa yenye ukame.

 

Wakulima wa mikoa hiyo wajengewe uwezo mkubwa wa kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua kwa njia malambo na mabwawa tofauti na hali ilivyo sasa ambapo maji mengi hupotelea ardhini bila kuyafanyia kazi zenye tija.

 

Sera ya Taifa ya Umwagiliaji ya Mwaka 2010 imezitaka halmashauri nchini kuweka mipango mkakati ya kuboresha sekta ya umwagiliaji na kuitengea bajeti ya kugharimia utekelezaji wake.

 

Mfano hivi karibuni, Halmashauri ya Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu ilipitisha rasimu ya mpango na bajeti yake ya mwaka 2020/2021, ambapo kwa upande wa sekta ya umwagiliaji imetenga Sh milioni 12.27 kwa ajili kugharimia usimamizi wa ukarabati wa skimu za Kinamwigulu, Ngongwa, Bukigi, Buyubi, Ijinga, Bukangilija na Pandagi.

 

(Uchambuzi wa Isaack Mbwaga kutoka Maswa)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages