NEWS

Tuesday 16 March 2021

Wachimbaji wadogo mgodi wa Marera waagizwa kuchimba vyoo

Wachimbaji wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Marera wilayani Tarime.

WACHIMBAJI wadogo katika mgodi wa dhahabu wa Marera uliopo katika bonde la mto Mara katika wilaya ya Tarime mkoani Mara - Tanzania, wameagizwa kuchimba vyoo mgodini hapo haraka iwezekanavyo.

 

Agizo hilo limetolewa na Afisa Tarafa ya Ingwe ulipo mgodi wa Marera, James Yunge, alipotembelea huko hivi karibuni, baada ya kubaini kuwa wachimbaji hao wanalazimika kujisaidia haja kubwa na ndogo vichakani kutokana na ukosefu wa choo mgodini hapo.

 

Hatua hiyo inalenga kuepusha uchafuzi wa mazingira katika maeneo ya mgodi wa Marera na bonde la mto Mara kwa ujumla. Mamia ya wachimbaji wadogo wanategemea mgodi huo kujipatia riziki kwa ajili yao na familia zao.

 

Waliopewa jukumu la kuchimba vyoo ni wamiliki wa mashimo ya uchimbaji wa dhahabu kwa ajili ya matumizi yao, wafanyakazi wao na wafanyabiashara wakiwamo wauzaji wa vyakula na vinywaji.

 

“Kuanzia sasa wadau wakubwa wenye leseni za uchimbaji katika mgodi huu kila mmoja achimbe choo, ninawapa muda wa wiki mbili kutekeleza agizo hili na nitakuja kufuatilia,” Yunge amewaagiza wachimbaji hao huku akitishia kufunga mgodi huo iwapo watakaidi agizo hilo.

Afisa Tarafa ya Ingwe, James Yunge (wa pili kulia) akitoa agizo la uchimbaji vyoo mgodini hapo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kerende ulipo mgodi huo, Mniko Magabe, amekazia agizo hilo akisema suala la kuchimba vyoo mgodini hapo ni la lazima.

 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata ya Kemambo ulipo mgodi wa Marera, Paul Maisori, ametaka utekelezaji wa agizo hilo ufanyike sambamba na kuwatengea mama lishe eneo maalumu - tofauti na hali ilivyo sasa ambapo kila mmoja anajichagulia aneo la kuendeshea shughuli zake mgodini hapo.

 

Naye Afisa Madini wa Mkoa wa Mara, Nyaisara Mgaya ameungana na viongozi hao kuwahimiza wachimbaji hao kutekeleza agizo hilo akisema suala la uchimbaji wa vyoo ni miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele katika migodi ya madini.

 

Wachimbaji wadogo wenye leseni katika mgodi huo wakiwamo Mwita Makindya na Marwa Mroni wamesema wako tayari kutekeleza agizo la kuchimba vyoo ndani ya muda wa wiki mbili.

 

Kwa upande wao, mama lishe katika mgodi wa Marera wakiwemo Agnes Chacha, Rhobi Msabi na Hawa Marwa wameeleza kupokea kwa furaha agizo la kutengewa eneo maalumu wakisema hatua hiyo itaepusha uchafuzi wa mazingira mgodini hapo.

 

Akitoa maoni yake kuhusu uchimbaji wa vyoo na utengaji wa eneo maalumu kwa ajili ya mama lishe, George Mkami ambaye ni mchimbaji mdogo anayefanya kazi katika shimo linalomilikiwa na Mwita Makindya, amesema utekelezaji wa maagizo hayo utawezesha shughuli za uchimbaji mgodini mgodini hapo kufanyika katika mazingira safi.

 

“Ninawapongeza viongozi wetu kwa kuliona tatizo lililokuwepo - japo wamechelewa kuchukua hatua. Binafsi ninaunga mkono maagizo hayo kwa sababu uchafuzi wa mazingira unahatarisha afya za wachimbaji katika mgodi huu,” amesema Mkami.

Sehemu nyingine ya wachimbaji wadogo katika mgodi huo.
 

Mchimbaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Saleh Hassan, ameshauri maafisa afya kuangalia uwezekano wa kwenda kuelimisha wachimbaji na wafanyabiashara katika mgodi huo umuhimu na faida za matumizi bora ya vyoo.

 

Hassan ameonesha wasiwasi kwamba baadhi ya watu mgodini hapo wanaweza kuendelea na mazoea ya kujisaidia vichakani hata baada ya vyoo kuchimbwa, kutokana na uelewa mdogo wa matumizi bora ya vyoo.

 

“Unajua kuna watu hawajui faida za matumizi ya vyoo, wamezoea kujisaidia ovyo vichakani hata wanapokuwa vijijini kwao. Kwa hiyo, ninadhani elimu ya matumizi ya vyoo itasaidia kufikia lengo la kuepusha uchafuzi wa mazingira katika mgodi huu na maeneo jirani,” amesisitiza mchimbaji huyo.

 

Mgodi wa Marera unatajwa kuwa miongoni mwa migodi inayozalisha kiwango kikubwa cha cha dhdhabu katika eneo la Nyamango wilayani Tarime lililopo ndani ya bonde la mto Mara.

 

(Habari na picha zote: Christopher Gamaina wa Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages