NEWS

Tuesday 16 March 2021

Wakazi bonde la mto Mara wanavyoadhimisha Wiki ya Maji

Wananchi wakishiriki kupanda miti katika eneo la bonde la mto Mara.
 

WANANCHI wanaoshi jirani na bonde la mto Mara na mto Mori wilayani Tarime, wamesema mwaka huu wataadhimisha Wiki ya Maji kwa kupanda miti kwenye maeneo ya hifadhi za vyanzo vya maji.

 

“Sisi tutapanda miti kwenye maeneo ya vyanzo vya maji ili kutunza na kuendelea kuhifadhi vyanzo vya maji na mazingira,” Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles ameiambia Mara Online News, leo Machi 16, 2021.

 

Siproza amesema wamekusudia kupanda miti 6,000 katika vijiji vitatu vilivyopo wilaya za Tarime na Rorya mkoani Mara. Vijiji hivyo ni Nkerege, Mara Sibora na Kwibuse.

 

“Tumepanga kupanda miti 2,000 kwa kila kijiji,” amesema Siproza ambaye ni mmoja wa wanawake walio mstari wa mbele katika kuhifadhi mto Mara upande wa Tanzania.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji ukanda wa Mara Kaskazini, Siproza Charles akizungumza na Mara Online News kijijini Mara Sibora.
 

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Watumia Maji Bonde la Mto Mori, Thomas Nkaina, amesema mbali na kupanda miti wataendelea kuelimisha wananchi juu ya utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira.

 

“Tulishapanda miti 20,000 na tunaendelea pia kutoa elimu juu ya uhifadhi wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla, na tayari tumefikia vijiji 10 kati ya 17 ambavyo ni lengo letu,” amesema Nkaina.

Upandaji miti ukiendelea katika bonde la mto Mara.
 

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) inawezesha jumuiya hizo za watumia maji kutekeleza wajibu wao wa kulinda na kuhifadhi mto Mara na mto Mori.

 

Mito hiyo inatiririsha maji kwenye Ziwa Victoria, hivyo ni mito muhimu kwa ustawi wa ziwa hilo, maisha ya wananchi na viumbe hai wengine.

 

Mfano, mto Mara unawezesha uwepo wa mamia ya nyumbu wanaohama kila mwaka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Mtoto akishiriki upandaji miti katika bonde la mto Mara.

Afisa Maji Dakio la Mara-Mori, Mhandisi Mwita Mataro amesema upandaji wa miti katika maeneo ya vyanzo vya maji utapewa kipaumbele katika maadhimisho ya Wiki ya Maji yanayoendelea nchini kote.

 

“Hata sasa hivi tunapanda miti kwenye kisima ambacho tumekikarabati,” Mhandisi Matato ameiabia Mara Online New leo asubuhi.

 

Amesema hivi karibuni ofisi yake imepanda miti 16,000 katika maeneo yaliyo jirani na mto Mara upande wa wilaya za Serengeti na Butiama.

 

Maadhimisho ya Wiki ya Maji nchini yameanza leo Machi 16 na yatahitimishwa Machi 22, 2021- yakiwa na kaulimbiu inayosema “Thamani ya Maji kwa Uhai na Maendeleo.”

Mojawapo ya miti ambayo ni rafiki kwa mazingira.
 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga amesema wiki hiyo itaadhimishwa kwa kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi 281 yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania zaidi ya trilioni moja.

 

Mhandisi Sanga ameongeza kuwa shughuli hizo zitafanyika sambamba na upandaji wa miti kwenye maeneo ya hifadhi za vyanzo vya maji.

 

Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Maji ameelekeza kwamba maadhimisho hayo hayatahusisha mikutano, warsha au makongamano.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga.

Kwa upande mwingine, Siproza amesema bado kuna hitaji la kuelimisha wananchi wanaoishi jirani na mto Mara umuhimu wa maadhimisho ya Wiki ya Maji.

 

Wananchi wengi hawajui maadhimisho ya Wiki ya Maji, elimu inatakiwa na ninyi vyombo vya habari msadie,” amesema mwenyekiti huyo wa jumuiya ya watumia maji ukanda wa Mara Kaskazini.

 

BODI YA MAJI BONDE LA ZIWA VICTORIA

Bodi ya Maji Bonde la Ziwa Victoria (LVBWB) ni taasisi inayojishughulisha na usimamizi wa rasirimali za maji, kutunza, kulinda na kudhibiti uchafuzi wa vyanzo vya maji katika Bonde la Ziwa Victoria.

Sehemu ya Ziwa Victoria jijini Mwanza

LVBWB ilianzishwa mwaka 2000 kwa mujibu wa Sheria Na. 42 ya Mwaka 1974 pamoja na mabadiliko yake yaliyofuata Sheria Na. 10 ya Mwaka 1981.

 

Lengo kuu la kuanzishwa kwa Bodi hiyo ni kuratibu, kusimamia na kuendeleza upatikanaji wa rasilimali za maji kwa mahitaji ya sasa na baadaye katika Bonde la Ziwa Victoria

 

Dira ya LVBWB ni rasilimali endelevu za maji kwa jamii na mazingira ya Bonde. Dhima ni kuwa na usimamizi wa pamoja wa rasilimali za maji ili kukidhi mahitaji ya kijamii, kiuchumi na kimazingira katika eneo la bonde hilo.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages