NEWS

Wednesday 17 March 2021

Sekondari ya Nyichoka yapokea msaada wa mabati 120 kutoka Grumeti Reserves

Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile (wa pili kushoto) akimkabidhi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma (wa nne kushoto), bati moja kati ya 120 yaliyotolewa msaada na kampuni hiyo kukamilisha uezekaji nyumba ya walimu katika Shule ya Sekondari ya Nyichoka, leo.

KAMPUNI ya huduma za kitalii ya Grumeti Reserves kupitia kampuni mwenza ya Grumeti Fund, imeipatia Shule ya Sekondari ya Nyichoka wilayani Serengeti, Mara msaada wa mabati 120 kwa ajili ya kukamilisha uezekaji wa nyumba ya walimu.

 

Akikabidhi msaada huo shuleni hapo leo Machi 17, 2021, Meneja Uhusiano wa Grumeti Fund, David Mwakipesile amesema mabati hayo yenye thamani ya Sh milioni 2.88 ni mwendelezo ya misaada ya kijamii wanayoelekeza kwenye vijiji 22 vilivyo jirani na eneo lao la uwekezaji.

 

“Pamoja na changamoto ya kibajeti, tumeamua kuwajali jirani zetu kwa msaada huu, ambao unatokana na faida ya uhifadhi wa wanyamapori, na tumefanya hivi ili kuwezesha wanafunzi wa shule hii kupata elimu bora,” amesema Mwakipesile.

Mwakipesile akizungumza wakati wa makabidhiano hayo.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyichoka wakifurahi na kupiga makofi wakati wa mapokezi ya msaada wa mabati hayo.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya uongozi na wanafunzi wa shule hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma ameishukuru kampuni hiyo na kutumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa wananchi kuiunga mkono katika utekelezaji wa shughuli zake.

 

“Tunapenda wawekezaji kama huwa, kwa kweli tumefurahi sana, wawekezaji wengine waige mfano huu wa Grumeti Reserves,” amesema Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Nyichoka, Modester Chaga ameishukuru kampuni hiyo na kuiomba isichoke kuendelea kutoa misaada ya kijamii kwa taasisi za umma katika vijiji mbalimbali.

 

Mapema, Diwani wa Kata ya Kyambahi ilipo shule hiyo, Herman Kinyariri, mbali na kushukuru, ametoa wito kwa wananchi na kampuni ya Grumeti Resevers kuimarisha uhusiano na ushirikiano wao kwa manufaa ya pande zote mbili.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma (kushoto) akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Nyichoka mara baada ya mapokezi ya msaada wa mabati 120 uliotolewa na kampuni ya Grumeti Reserves.
 

Naye Mwakilishi wa Mbunge wa Serengeti, Muhogo Mugabo amesema msaada huo unadhihirisha jinsi kampuni hiyo inavyothamini na kujali jirani zake wakati wa mahitaji muhimu.

 

Mabati hayo yanatarajiwa kukamilisha uezekaji wa nyumba kwa ajili ya familia za walimu wawili wa shule hiyo.

 

(Habari na picha zote: Mara Online News)

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages