
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
----------------
Dodoma
----------------
Tanzania na Marekani zimekubaliana kuimarisha ushirikiano katika utafiti wa madini ya kimkakati ili kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa taifa.
Januari 21, 2026 nchi hizo zilifanya mazungumzo ya pamoja jijini Dodoma, Tanzania kuhusu jinsi Wizara ya Nishati na Madini ya Marekani itakavyosaidia uwezo wa utafutaji madini na usimamizi wa sekta hiyo.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andrew Lentz.
Moja madini ya kimkakati yatakayofanyiwa utafiti ni aina ya kinywe.
Kwa miongo kadhaa, Marekani imekuwa mshirika mkubwa wa maendeleo ya Tanzania kupitia misaada ya kiufundi na fedha.
Sekta zilizofaidika na misaada ya Marekani ni elimu, kilimo, miundombinu, afya, utawala bora na ujenzi wa demokrasia.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mavunde alisema misaada ya kiufundi ya Marekani ni kielelezo cha dhamira ya nchi hiyo katika kuimarisha sekta ya madini na kuunga mkono agenda ya maendeleo ya Tanzania.
Alizielekeza Taasisi ya Ikolojia na Utafiti Madini Tanzania (GST) na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kutumia fursa hiyo kuongeza ujuzi.
Ushirikiano wa Tanzania na Marekani katika sekta ya madini unatarajiwa kuibua migodi mikubwa ya madini ya kinywe katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Waziri Mavunde alisema Tanzania itakuwa miongoni mwa nchi zinazozalisha kinywe duniani na kwamba kufikia mwaka 2050 uhitaji wa madini hayo utafikia tani milioni 4.5.
No comments:
Post a Comment